VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Wednesday, December 30, 2015

Waziri Mkuu Aibua Ufisadi Kigoma......Atoa siku Mbili Kwa Katibu Tawala wa Mkoa Kukamilisha Uchunguzi ,Ataka Apewe Taarifa ya Maandishi Januari Mosi, 2016



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.

“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

“Nataka kujua nani alifanya tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua hatua za kinidhamu,” alisema.

Viongozi walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng. Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.

Kuhusu uuzwaji wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst), Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015 akitaka viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na mchakato huo usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja pekee.

Tuhuma nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa maabara.

Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).

Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.

Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na Mhasibu Mkoko.

Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
(mwisho)


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATANO, DESEMBA 30, 2015
VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Polisi Ahukumiwa Kifungo cha Maisha Jela Kwa Kubaka na Kumlawiti Mtoto


MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, imemhukumu askari polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, G 9762 PC Daniel (24) kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na makosa ya kubaka na kumlawiti mtoto wa miaka 13.
Mbali na kifungo hicho, mtuhumiwa huyo ameamriwa kulipa fidia ya Sh milioni 2 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa baada ya kukamilika ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi wanne.
“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kubaka na kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti mtoto na baadaye atalipa fidia ya Sh 2,000,000 ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Mkasiwa.
Katika utetezi wake,  mtuhumiwa kupitia kwa wakili wake ambaye alitajwa kwa jina moja la Manzi, alidai kosa hilo ni la kwanza na ni kijana mdogo ambaye  ni  nguvu kazi ya taifa, pia alifanya kosa hilo akiwa amelewa, hivyo hakujua alichokuwa akikifanya.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elik Shija, alidai  hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa, hivyo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
A ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Monday, December 28, 2015

Wachimbaji Kadhaa Wafunikwa Na Kifusi Chunya, Mkoani Mbeya Leo


Wachimbaji kadhaa wamefukiwa na kifusi katika kijiji cha Sangambi wilaya ya Chunya mkoani Mbeya hivi sasa, Juhudi za kuokoa uhai wao zinaendelea muda huu.

Tinga tinga likiendelea na juhudi za uokoaji hivi sasa.
VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Saturday, December 26, 2015

Picha: Lowassa Aanza Kuchunga Ng'ombe Kama Alivyoahidi


Aliyekuwa mgombea wa uraisi kwa mwavuli wa UKAWA ndugu Edward Lowasa  akichunga ng'ombe zake huko Handeni mkoani Tanga. 
 
Lowassa yuko mapumzikoni na familia yake katika shamba lake la mifugo lililopo eneo la Mzeri,Handeni mkoani Tanga

VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Monday, December 21, 2015

Rais Magufuli akutana na Maalim Seif Ikulu leo

Rais Magufuli amekutana na kuzungumza na mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif juu ya mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar
  
                     VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Mkuu wa Upelelezi TANAPA Achinjwa Kinyama Kama Kuku na Mwili Wake Kuwekwa Katika Buti la Gari yake

POLISI mkoani Arusha imewatia mbaroni watu wawili wanaohusishwa na tukio la kuuawa kinyama kwa kuchinjwa shingo kwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Stephen Kisamo.

Kifo cha Kisamo kinahusishwa na mambo mengi yakiwemo vita ya kupambana na ujangili, ikielezwa mkuu huyo alikuwa na siri nzito juu ya watu wanaojihusisha na ujangili wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Arusha, watumishi wa serikali na wanasiasa.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Arusha zilieleza tayari imewatia ndani watu wawili ambao ni marafiki wakubwa wa Kisamo na wanajua siri nzito kutokana na kunaswa kwa mawasiliano ya simu ya kiganjani kati ya marehemu na watu fulani muda mfupi kabla ya mauti kumfika ambao polisi inawachunguza kwa karibu.

“Wasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas sisi tumeshakamata watu wawili wa karibu na marehemu na sms na mawasiliano yanatia shaka, lakini ukweli utajulikana muda si mrefu,” kilieleza chanzo chetu cha habari ndani ya Jeshi la Polisi.

Kamanda Sabas alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo Desemba 18, mwaka huu asubuhi katika eneo la Kikwakwaru jijini Arusha muda mfupi baada ya Kisamo kutoka nyumbani kwake akiwa na gari aina ya Mazda.

Sabas alisema siku hiyo hiyo jioni alifika kituoni hapo mke wa marehemu na kueleza juu ya kutoweka kwa mumewe ambapo mara moja polisi walianza kufuatilia jambo hilo bila mafanikio.

Kamanda Sabas alisema usiku, Polisi ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema wa eneo hilo la Kikwakwaru kuhusu kuonekana kwa gari hilo likiwa limeegeshwa maeneo hayo kwa muda mrefu bila kuonekana mtu yeyote ambapo walifika na kulikuta gari hilo, lililovutwa hadi katika Kituo Kikuu cha Polisi usiku huo na baadaye lilitambuliwa na mke wa Kisamo.

Baadaye walirejea eneo la tukio kwa lengo la kutafuta mwili wa marehemu huyo, lakini hawakufanikiwa kuupata mwili wala kumuona kachero huyo ambapo walilazimika kuomba ruhusa ya kupekua gari hilo.

Alisema baada ya kuomba ruhusa hiyo, mke wa marehemu alipowasilisha ufunguo wa akiba wa gari na Polisi walipofungua na kuanza upekuzi walikuta mwili wa marehemu ukiwa umekunjwa kwenye buti, huku shingo yake ikiwa imechinjwa eneo la nyuma ya shingo yake.

Aidha, Kamanda Sabas alisema kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, mumewe alikuwa mgonjwa na alikuwa akijiandaa kwa safari ya India kwa matibabu, hivyo kabla ya tukio walidhani alitekeleza gari baada ya kuzidiwa na ugonjwa.
Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru
.

Saturday, December 19, 2015

Majipu ya Tanesco Yaendelea Kutumbuliwa...Wengine 10 Wasimamishwa Kazi Kwa Upotevu wa Mapato zaidi ya Sh Mil 100

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felchesmi Mramba, amewasimamisha kazi maofisa 10 wakiwamo wahasibu waandamizi na mafundi kwa kusababisha upotevu wa mapato zaidi ya Sh.milioni 100.

Hasara hiyo ilitokea katika mfumo wa mita kupitia minara ya simu za mkononi na faini Sh. milioni 198.1 za wateja waliobainika kuiba umeme kwa kuchakachua mita zao.

Hata hivyo, shirika hilo limefanikiwa kuokoa fedha hizo zilizotokana na umeme wenye thamani ya Sh. 100,248,386.42 uliotumika bila kulipiwa pamoja na faini kutoka kwa wateja waliojihusisha na wizi wa umeme Sh.
198,105,928.68.

Kadhalika, shirika baada ya kufanya msako mkali limefanikiwa kukamata taasisi binafsi na za serikali pamoja na watu binafsi wakijihusisha na kuhujumu shirika hilo,ikiwemo Shule ya Sekondari ya Jangwani (Sh. 11,023,238.00), Diwani wa Kata ya Sinza C, Joseph Marandu (Sh. 3,443,555.00), Royal Oven Bakery Kawe, (Sh. 4,112,614.00), Havan Hotel, Mbezi Beach (Sh.1,847,913.00) na Kampuni ya Simu ya Viettel Mtwara (Sh. 524,554.76).

Wengine ni, Kampuni ya Saffa Petroleum ya Mkoani Pwani (Sh. 16,105,235.00), Msanii wa Filamu Nchini, Wema Sepetu (Sh. 8,200,496.20) na Kampuni ya Leadcom (Sh. 13,694,632.81).

“Zoezi hili ni endelevu kwa nchi nzima na tutaendelea kuwakamata, kuwatangaza na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale watakaobainikiwa kulihujumu shirika hatutaogopa wadhifa wala umaarufu wa mtu ama taasisi” alisema Mramba katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema mapema Desemba 6, mwaka huu alitoa taarifa kwa wale wote wanaojihusisha na wizi wa umeme ama wenye mita zenye matatizo, lakini walijisalimisha ni watu 30 na kati ya watu 2,156 waliokaguliwa 138 walikutwa na dosari mbalimbali katika mita zao na walilipishwa faini.

Akifafanua, alisema fedha zinazotakiwa kulipwa ni Sh. milioni 198.1 na zilizokwishalipwa ni Sh. milioni 44.9 wakati waliofikishwa kwenye vyombo vya sheria ni watu 37 kwa makosa mbalimbali. Akizungumzia kuhusu hatua atakazowachukulia watumishi 10 aliowasimamisha kazi, Mramba alisema uchunguzi unaendelea na fedha wanazodaiwa kuzifanyia udanganyifu zitalipwa na kampuni ya simu husika.

Mramba alisema ili kuhakikisha kero za huduma zinamalizika, katika kila ofisi ya kitengo cha dharula kutakuwa na  Ofisa wa huduma kwa wateja na mhandisi ambao watasimamia muda na ubora wa huduma wanazopata wateja baada ya kutoa taarida za dharura.

“Kuanzia sasa kazi ya mafundi inapokamilika maofisa hawa niliowataja watawajibika kuwapigia simu wateja waliotoa taarifa kuhakiki kama kazi zimefanywa kwa wakati na mteja ameridhika … utaratibu huu utaanza leo (jana),” alisema Mramba.

Friday, December 18, 2015

Tazama Picha Zikionyesha Unyama Unaofanyika Nchini Burundi, Watu Wanauawa Kama Wanyama

Umoja wa Afrika(AU) umeahidi kuhakikisha mauaji ya kimbari hayatokei Burundi. Wasema kuna uwezekano wa vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Kuanzia mwezi Aprili mwaka huu, watu takribani 400 wamepoteza maisha nchini Burundi kutokana na vurugu zinazoendelea
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Thursday, December 17, 2015

Zitto Kabwe Afunguka Mazito..Awataka Baadhi ya Wanasiasa Kuacha Siasa za Porojo

Mbunge wa Kigoma mjini kupitia chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amefunguka na kuwataka baddhi ya wanasiasa kuacha siasa za porojo na kuangalia masuala ya msingi na sio uteuzi wa Prof. Sospeter Muhongo.

Zitto Kabwe ameyasema haya kupitia mtandao wake wa kijamii wa facebook siku kadhaa baada ya Mbunge wa Kibamba kupitia tiketi ya Chadema . John Mnyika kudai kuwa atafufua sakata la Escrow bungeni kufuatia uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli kumteua Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo.

"Prof. Sospeter Muhongo alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa sakata la ‪#‎TegetaEscrow‬. Kamati ya Bunge ilipendekeza na Bunge kuazimia kuwa Muhongo avuliwe madaraka yake ya Uwaziri. Prof. Muhongo alijiuzulu. Akafanyiwa uchunguzi na Kamishna wa Maadili kutamka kuwa hakukutwa na kosa la kimaadili" Alisema Zitto Kabwe

Lakini Mbunge huyo alizidi kusikitiza kuwa "Unajengaje hoja kuwa hana haki ya kuteuliwa kuwa Waziri? Keshaadhibiwa kwa kosa la awali, kwa kujiuzulu. Sheria ipi inasema hana haki ya kuteuliwa tena? Niliongoza Kamati ya PAC. Nina uhakika Waziri muhongo kwenye sakata lile alishauriwa vibaya na kujikuta anatetea ubadhirifu. Lile nifunzo kubwa kwake na ninavyomuona sasa hatarudia tena makosa yale. Kuna mambo ya msingi lazima afanye sasa

1) Azuie kuanzia sasa malipo ya 'capacity charges' kwa kampuni ya kitapeli ya IPTL na atumie sheria kutwaa mitambo ya IPTL na kumilikisha TANESCO
2) Amtake Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kumkamata mara moja anayejiita mmiliki wa IPTL na afunguliwe mashtaka ya utapeli, wizi wa udanganyifu na uhujumu uchumi; huyo mmiliki na washirika wake ambao ni raia wa Tanzania

3) Amtake Gavana wa Benki Kuu na FIU kuichukulia hatua za kisheria Benki ya Stanbic ikiwemo kupiga faini ya kurejesha fedha zote zilizokua kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Hizo ndio hoja za msingi na sio uteuzi wa Prof. Muhongo. Mwenye ushahidi dhidi ya Muhongo si aende Mahakamani? Tuache siasa za porojo porojo" Alisisitiza Zitto Kabwe.

Wednesday, December 16, 2015

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Afanya Ziara ya Kushtukiza Hospitali ya Muhimbili Leo na Kukuta Mashine za CT Scan na MRI Zimeharibika Tena

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili leo na kukuta mashine za CT Scan na MRI hazifanyi kazi.

Katika ziara hiyo aliyoifanya asubuhi ya leo, alikutana na mzee wa miaka 90 ambaye alikuwa akisubiri huduma hiyo tangu jana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Wa Hospitali hiyo, Lawrence Museru, mashine hizo ziliharibika tangu juzi na hivyo huduma zilisimama tangu jana asubuhi.

Tatizo kubwa katika machine ya CT Scan picha hazisomeki vizuri na MRI imeharibika spea ambazo kwa mujibu wa uongozi wa hospitali hiyo, matengenezo yanaanza leo.

Hata hivyo, Mwalimu ameagiza uongozi wa hospitali hiyo ya rufaa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa mashine hizi zinarudi katika hali yake ya kawaida.

Mashine hizo zimeendelea kuwa changamoto kwa hospitali hiyo licha ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza na kukuta hali kama ya leo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Tuesday, December 15, 2015

Tanesco Bado Mnafungulia Maji Usiku Katika Mabwawa Yenu? Mvua ni Nyingi Mgao Ukome Basi!

Kuna mkuu mmoja aliwatuhumu Tanesco kwamba huwa wanafungulia maji usiku ili mabwawa yaonekane hayana maji, Mgao uanze wapige dili za mafuta na Jenereta,Mwaka huu mvua ni nyingi sana, hatutarajii muendelee kutukatia umeme kama mnavyofanya katika mikoa ya Arusha na Mwanza...natoa wito kama kuna wanaofungulia maji bado wakamatwe.....

Wanne Wakataa Uwaziri wa Magufuli Wakihofia Kushindwa Kuendana na Kasi Yake


WABUNGE wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, wabunge wamedai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wizara 4 zilizokosa Mawaziri
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.
Kinana atoboa siri
Mwishoni mwa wiki akiwa mkoani Arusha, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alitoa siri ya wabunge wanne ambao walipigiwa simu za uteuzi wa uwaziri, lakini walikataa kwa hofu ya kushindwa kwenda na kasi ya Rais Magufuli.
Alisema anachoamini ni kwamba Rais John Magufuli, atakuwa aliwaeleza baadhi ya wabunge kuhusu nia yake ya kuwateua katika nafasi hizo, lakini wao wakamwomba asiwape majukumu hayo kwa kuwa hawana uhakika wa kwenda na kasi anayohitaji katika Serikali yake.
Kinana alisema kinachojitokeza sasa ni kama alivyoshauri Rais Magufuli kuwa si vema kwa waziri aliyeteuliwa kufanya sherehe nyumbani kwake na kuita marafiki kwa kuwa wana mzigo mzito katika kuwatumikia wananchi.
“Ni vema mawaziri hawa wakafanya maombi kwa kuwaita au kuwafuata viongozi wa dini kwani wana kazi ngumu kulingana na nia njema aliyonayo Rais Magufuli katika kupambana na masuala ya ufisadi.
“… kazi ya kupambana na ufisadi kamwe si rahisi hadi kushangilia uteuzi, lengo kubwa ni kuwaletea wananchi maendeleo kupitia ubinafsishaji wa viwanda kutoka kwa watu waliomilikishwa na kuviua,” alisema Kinana.
Katibu mkuu huyo wa CCM, alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi dunaini, hali ya kuwa wagonjwa hawana dawa.
“Nyingine ni Wiki ya Maji, mnafanya maadhimisho huku watu hawana maji, Wiki ya Maziwa wakati wafugaji wamekonda na mifugo imekonda haitoi maziwa, fedha hizo zitumike kwa mambo mengine,” alisema Kinana.

Monday, December 14, 2015

Wakulima Na Wafugaji Wauana na Kujeruhiana Morogoro......Waziri Mwigulu Afika Kutatua Ugomvi


Mkulima mmoja ameuawa, mwingine amejeruhiwa wakiwemo askari  polisi wawili kwenye mapigano dhidi ya wafugaji wa kimang’ati kwenye kijiji cha Dihimba Turiani, mkoani Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa amesema mapigano hayo yametokea baada ya wafugaji kutaka kuwachukua kwa nguvu ng’ombe zaidi ya 150 waliokuwa wakishikiliwa na wakulima kwenye ofisi ya kijiji hicho.

Mkwasa amesema siku ya tarehe 11 mwezi huu, mkulima mmoja aliyejulikana kwa jina la Bakari Mulunguza alikuta ng’ombe zaidi ya 150 wakila shambani kwake pasipo kuwa na mchungaji wa ng’ombe hao, ndipo Mulunguza alipoomba msaada kutoka kwa wakulima wenzake kwa pamoja waliwaswaga ng’ombe hao hadi kwenye ofisi ya serikali ya kijiji.

Amesema wakulima hao waliamua kuchukua uamuzi huo ili mwenye ng’ombe ajitokeze na kupigwa faini kutokana na uharibifu uliosababishwa na ng’ombe hao. Alisema siku iliyofuata ya tarehe 12, ndipo alipojitokeza mfugaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Shaabani Ikeli na kudai kuwa yeye ndiye mmiliki wa ng’ombe hao.

“Serikali ya kijiji ilimtaka mfugaji huyo kulipa faini ya Shilingi laki mbili kama fidia kutokana na uharibifu uliosababishwa ; mfugaji huyo alikubali na kuahidi kuwa angelipa faini hiyo, lakini cha kushangaza alirudi na kundi kubwa la vijana wafugaji wakitaka kuwachukua ng’ombe kwa nguvu, ndipo mapigano yalipotokea,” alisema Mkwasa.

Alimtaja aliyeuawa kuwa ni Mohamed Musa (43) mkulima wa kitongoji cha Kaole, na aliyejeruhiwa ni Charles Paulo (35) ambaye amelezwa hospitali ya Bwagala Turiani kwa matibabu.

Mkwasa amesema kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wakulima ambao walilipa kisasi kwa kuwakatakata miguu na sehemu mbalimbali za miili ng’ombe 150. Alisema polisi walifika eneo la tukio na kudhibiti vurugu hizo; amesema polisi wawili wamejeruhiwa kweye mapigano hayo.
Mwigulu Nchemba  Afika Eneo La Tukio 
Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji Mh. Mwigulu Nchemba leo hii amefika katika eneo la tukio.Akizungumza na wananchi hao Waziri  Nchemba alikuwa na haya ya kusema;

"Natoa rai kwa Wananchi hususani wa jamii ya Wafugaji na Wakulima, hakuna ardhi au mnyama mwenye thamani sawa na maisha ya mwanadamu yeyote yule,njia bora na salama ya kutatua migogoro hii inayohusisha wakulima na wafugaji ni kufuata taratibu za kuonana na uongozi wa serikali wa eneo husika hatua kwa hatua".

Pia Mh. Mwigulu amesema ameagiza ulinzi maeneo yote yenye migogoro, pili wahakikishe waliosababisha maafa wanakamatwa mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sharia na  kwa walio jeruhiwa, ameagiza wapatiwe matibabu kwanza bila kuchelewa na hatua za kisheria kwa wenye hatia zifuate.

"Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mikononi, tunakwenda kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro hii kwa kila kijiji zitakazohusisha pande zote mbili ili kubaini wavamizi wa maeneo na kuwachukulia hatua za kisheria."

 

Thursday, December 10, 2015

Breaking News: Rais Magufuli Atangaza Baraza Lake la Mawaziri

Ndugu waandishi wa habari na watanzania kwa ujumla, ninawasalimu sana. Nawakaribisha katika kikao hiki cha kutangaza baraza la mawaziri.

Tutakuwa na mawaziri 19, kuna baadhi ya wizara zitakuwa na mawaziri na hazitakuwa na manaibu waziri. Lengo ni kuwa na baraza dogo kupunguza gharama.

Zilitengwa bilioni 2, mawaziri watakapoteuliwa waende semina elekezi, baraza nitakaloliteua halitakuwa na semina elekezi na fedha tutaelekeza sehemu nyingine kama ni madawati au kwenye elimu bure.

Wizara ni 18 lakini Mawaziri ni 19 kwa sababu wizara ya Ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa Umma naiunganisha na Utawala bora hivyo itakua na mawaziri wawili. Wizara ni kama ifuatavyo;

1.Wizara ya Ofisi ya Rais,Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora.
Mawaziri - George Simbachakene  na Angella Kairuki
Naibu Waziri - Sumeilam Jafo
 
2.Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Raisi, Muungano na Mazingira
 
Waziri - January Makamba
Naibu Waziri – Luhaga Jerrson Mpina

3.Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu
 
Waziri - Jenista Muhagama
MaNaibu – Dkt. Possy Abdallah na Anthony Mavunde.

4.Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
 
Waziri - Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri - William Ole Nasha

5.Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 
Waziri : Bado hajapatikana.
Naibu Waziri – Inj. Edwin Ambandusi Ngonyani

6.Wizara ya Fedha na Mipango
 
Waziri: Bado hajapatikana.
Naibu Waziri - Ashantu Kizachi

7.Wizara ya Nishati na Madini
 
Waziri - Prof. Mwigalumi Muhongo.
Naibu Waziri - Medalled Karemaligo.

8.Wizara ya Katiba na Sheria,
Waziri - Harrison Mwakyembe

9.Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
 
Waziri - Dk. Augustino Mahiga
Naibu Waziri – Dkt. Susan Kolimba.

10.Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Waziri - Dk. Hussein Mwinyi

11. Wizara ya Mambo ya Ndani
Waziri - Charles Kitwanga.

12.Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 
Waziri - William Lukuvi
Naibu Waziri - Angelina Mabula

13. Wizara ya Maliasili na Utalii
Waziri: Bado hajapatikana.
Naibu Waziri– Inj. Ramol Makani

14: Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
 
Waziri: Charles Mwijage.

15: Wizara ya Elimu,Sayansi Teknolojia na Ufundi.
 
Waziri: Bado hajapatikana.
Naibu Waziri – Inj. Stella Manyanya

16: Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
 
Waziri - Ummy Mwalim
Naibu Waziri –  Dkt. Hamis Kigwangala

17: Wizara ya Habari, Utamadu, Wasanii na Michezo
 
Waziri - Nape Nnauye
Naibu Waziri - Anastasia Wambura.

18:Wizara ya Maji na Umwagiliaji
 
Waziri – Prof. Makame Mbarawa
Naibu  Waziri– Inj. Isack Kamwela

Monday, December 7, 2015

NEC Yatoa Tamko Kuhusu Uchaguzi Wa Wabunge Arusha Mjini Na Handeni.

Na Jacquiline Mrisho-Maelezo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza siku ya kupiga kura kwa baadhi ya majimbo ambayo uchaguzi wake ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali
 
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametaja siku hiyo ya uchaguzi itakuwa Disemba 13, mwaka huu.

“Natoa rai kwa Wananchi wote waliojiandikisha kama wapiga kura katika Majimbo na Kata husika kujitokeza katika vituo walivyojiandikishia ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka” amesema Lubuva.

Jaji Lubuva aliyataja majimbo hayo ambayo wananchi watapiga kura za kuchagua Wabunge kuwa ni Majimbo ya Arusha Mjini na Handeni Mjini ambapo uchaguzi wa Madiwani katika kata  za Mvomero, Ipala na Nyamwilolewa nao utafanyika siku hiyo.

Aidha, Jaji Lubuva  amesisitiza kuwa, taratibu zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 mwaka ndizo zitakazotumika kwenye uchaguzi kwenye majimbo hayo na kata hizo.

Kwa ufupi, Jaji Lubuva alikumbushia baadhi ya taratibu hizo zikiwemo za mpiga kura kubeba kadi yake ya kupigia kura pindi aendapo kupiga kura, mawakala wa vyama vya siasa lazima wawepo kwenye kila kituo na pia Maafisa Uchaguzi  kufungua kituo na kufunga kwa muda uliopangwa na Tume.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, uchaguzi wa Wabunge na Madiwani wa Majimbo 7 pamoja na Kata 35  ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vifo na vurugu.

Thursday, December 3, 2015

Rais Dkt. Magufuli atoa siku saba kwa wafanyabiashara wakwepa kodi.



Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt.John  Pombe  Magufuli amewapa siku saba kuanzia tarehe 03/12/2015 wafanyabiashara wote ambao waliingiza mizigo yao bila kulipa kodi wakalipe kwani baada ya hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria
 
Hayo  yamesemwa leo Ikulu  jijini Dar es Salaam na Mheshimiwa Rais katika mkutano wake na wadau wa sekta binafsi  alipoamua kufanya mazungumzo nao pamoja na kuwasikiliza maoni  yao ikiwa ni sehemu ya ahadi zake katika kipindi cha kampeni za kuomba kura za kiti cha Urais,lengo likiwa ni kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Rais  aliendelea kusema kuwa katika kipindi hichi cha miaka mitano amedhamiria kuijenga nchi na watu wasimuelewe vibaya kwa maamuzi anayofanya kwani ni kwania njema ya kuleta maendeleo na siyo ujeuri.

“Tutaangalia namna ya kupunguza utitiri wa ushuru katika bidhaa mbalimbali,mfano katika kipindi cha kampeni niligundua katika Mkoa wa Kagera na Kilimanjaro wanakolima zao la Kahawa,wamekuwa wakitozwa tozo  26 kwa zao hilo na hiyo imechangia kusababisha wafanyabiashara wa zao hilo kufanya biashara haramu ya kupeleka zao hilo kwa magendo kuuza  katika nchi jirani”,alisema Mheshiwa Rais Dkt. Magufuli.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Dkt.Magufuli amewaahidi wadau wasekta binafsi ushirikiano mkubwa kwani anatambua mchango wao katika kukuza uchumi na pia amewataka wadau hao kuwa wazalendo na kuliacha kukwepa kulipa kodi ili tuweze kujenga taifa lenye maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli  ameendelea kusema kuwa kama kutakuwa na mfayabiashara yeyote  atakayetaka kuwekeza  na akakwamishwa na  mtu aliyechini ya uteuzi wake  basi mtu huyo ataondoka kwani sasa ni wakati wa wadau wa sekta binafsi kuanza kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyo toa ajira.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amewapa mawazo ya kibiashara wadau wa sekta binafsi kuanzisha kampuni ya kutenganisha udongo unaotoka kwenye machimbo ya madini,kuanzisha viwanda vya samaki pembezoni mwa bahari pamoja na kutengeneza samani zitokanazo  na mazao ya misitu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw.Regnald Mengi amesema kuwa wako tayari kumpa ushirikiano mkubwa  Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha uchumi watanzania unakuwa kwa haraka na pia amemuomba mheshimiwa rais kuendelea kukemea masuala ya rushwa  pamoja kusaidia kupunguza utitiri wa kodi

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Reginald Mengi akiongea katika mkutano huo na kumuahidi Rais Dkt. Magufuli ushirikiano katika kutekeleza yale anayodhamiria kwenye serikali yake ikiwemo kusimamia ulipaji kodi kwa dhumuni la kuiinua Tanzania kiuchumi
 

Baadhi ya Wadau wa Sekta Binafsi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mkutano huo Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
 

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Reginald Mengi akimpongeza  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipomaliza kutoa hotuba kwa wajumbe wa Sekta Binafsi nchini Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimueleza Jambo Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Reginald Mengi wakati wa Mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi nchini Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.