Kwa ufupi
Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray alisema: “Hili si jambo
jipya kwa kuwa lilishawahi kutokea lakini baada ya kuona halina maana
wengine tuliamua kujitoa… tumekaa pembeni tuone watakapofika.
Kauli ya
Mbowe ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa imekuja huku kukiwa na maoni
kutoka kwa watu mbalimbali wakiukosoa ushirikiano huo na kwamba
hautadumu kutokana na viongozi wengi wa kisiasa nchini kuwa na tabia za
kutanguliza masilahi binafsi.
Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa kikwazo kwa
viongozi hao ni suala la ruzuku ambayo hutolewa kwa kuzingatia wingi wa
wabunge na idadi ya kura za mgombea urais pamoja na suala la mgawanyo wa
majimbo ya uchaguzi hasa katika maeneo ambayo chama zaidi ya kimoja
vina nguvu.
Hata hivyo, jana Mbowe alipuuza dhana hiyo kwa
kusema: “Historia ya upinzani nchini imetufundisha mengi na tutakuwa
wajinga kama muda wote hatukuweza kujifunza.
“Tunafahamu na tunatambua wapo watu ambao
walijitahidi sana kutugawa na kutugombanisha, lakini naomba Watanzania
watambue kwamba katika hatua hii hatutakubali kugawanyika tena wala
kugombana tena.”
Juzi, vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR
Mageuzi, CUF na NLD vilisaini makubaliano ya kushirikiana ikiwa ni
pamoja na kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo tukio
lililofanyika kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani, Dar
es Salaam.
Akizungumzia suala la ruzuku, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema: “Tuna uzoefu wa miaka 24 sasa katika siasa
za vyama vingi na siasa za ushindani, kwa hiyo suala la ruzuku haliwezi
kutugombanisha kwa sababu tumeamua kwa dhati kuweka mbele masilahi ya
nchi.
“Hilo linawezekana kabisa, tumeonyesha mfano kwa
sababu pamoja na umaskini wetu, tulisusia Bunge la Katiba na tukakosa
zaidi ya Sh3 bilioni. Hii haimaanishi kwamba watu wetu hawakuwa
wakihitaji hizo fedha, lakini ni suala la msimamo tu kuhusu masilahi
mapana ya nchi.”
Alisema mambo yote yanayofanyika ndani ya
ushirikiano huo yamekuwa yakiratibiwa na timu za wataalamu wakiwamo
wanasheria kisha mapendekezo husika kuridhiwa na viongozi wakuu, hivyo
hakuna shaka kwamba kila jambo litafuata utaratibu huo.
“Tunao wataalamu wengi wakiwamo wanasheria, kwa
hiyo hakuna kitakachoshindikana maana sisi hatuongozwi na matakwa ya
ruzuku, tunaongozwa na dhamira safi za kutanguliza masilahi mapana ya
nchi,” alisisitiza.
Muungano wa Ukawa dhidi ya CCM, ni matokeo ya
misuguano iliyojiri wakati wa mchakato wa Katiba. Hatua ya kwanza
ilianza kwa Mbowe kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli, likiwashirikisha
wabunge kutoka vyama hivyo isipokuwa NLD ambacho hakina mwakilishi
bungeni.
No comments:
Post a Comment