Wakati kukiwa na taarifa zinazosambaa mtandaoni zikimuhusisha Dk Willibrod Slaa na akaunti ambayo imekuwa ikitoa msimamo wake wa kujitenga na shughuli za siasa pamoja na Ukawa, katibu huyo mkuu wa Chadema amekanusha taarifa hizo akisema hajawahi kuwa na akaunti ya twitter.
Dk
Slaa, aliyekuwa anatajwa kuwa mgombea urais wa Chadema, hajaonekana
hadharani katika matukio makubwa ya kichama tangu Chadema na Ukawa
walipomkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumteua kuwa
mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda umoja huo.
Mara
ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za chama hicho ni katika kikao cha
Kamati Kuu wakati Lowassa alikaribishwa kufanya majadiliano na kujibu
hoja za wajumbe.
Lakini
baada ya hapo Dk Slaa hakuonekana wakati wa kutambulishwa kwa Lowassa
kwa waandishi wa habari, tukio la kuchukua na kurudisha fomu za urais
ndani ya chama na tukio la juzi la kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati
hayo yakiendelea, kuna akaunti ya twitter yenye jina la “Dr Willibrord
Slaa” ambayo imekuwa ikitoa kauli mfululizo zikiwa na ujumbe mbalimbali
unaoendana na mazingira aliyomo sasa mwanasiasa huyo.
Agosti 10, kulitumwa ujumbe zaidi mara 10, mmojawapo ukijaribu kuwaaminisha watu kuwa hiyo ni akaunti halisi ya Dk Slaa.
“Ndugu
zangu Watanzania, hii ni akaunti yangu rasmi, bila shaka yoyote na
naomba ninachoandika hapa kifikishwe kwa Watanzania popote walipo,” unasema ujumbe huo.
Taarifa
nyingine zilizotumwa kwenye akaunti hiyo ya twitter ni pamoja na ile
iliyoeleza kuwa Dk Slaa ameomba ulinzi kutoka nchi na mashirika ya
kimataifa na atazungumza kupitia runinga na redio pindi atakapopata
ulinzi.
Akizungumzia sakata hili jana, Dk Slaa alisema hajawahi kutuma taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii.
“Sijawahi ku-operate (kuendesha) kitu chochote kwenye akaunti ya twitter, sina akaunti kama hiyo,” alisema Dk Slaa.
Mbali
na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli
yake ya wiki iliyopita kuwa atatoa msimamo wake muda muafaka
utakapofika, baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma yake ndani ya Chadema
na kisiasa kwa ujumla.
“Subira yavuta heri, sasa ili uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa
ni wapi alipo kwa sasa, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini
akasisitiza kuwa ipo siku ataweka wazi mustakabali wake kisiasa.
Dk
Slaa alisema yeye na mke wake Josephine Mushumbusi wanatarajia kusafiri
kwenda nje ya nchi katika siku chache zijazo, ingawa hakuweka wazi nchi
anayotarajia kuitembelea, lakini akasema atarejea baada ya wiki moja.
No comments:
Post a Comment