Aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
amesema hana mpango wa kustaafu siasa kwa sababu haina mwisho.
Pia,
amesema kwa sasa anafanya kazi ya uandishi wa vitabu kwa lengo la
kuwashirikisha na kuwarithisha Watanzania mazuri aliyonayo baada ya
utumishi wake wa kisiasa wa miaka 35.
Amesema anaandaa vitabu vinne vyenye maudhui tofauti. “Hilo
la kuandika vitabu nimeshalianza, nina vitabu zaidi ya 265 nimehifadhi
na kuvisoma katika maktaba yangu kuhusu mambo mbalimbali ya dunia, nami
ninatengeneza vinne, muda ukifika nitatoa taarifa,” alisema Membe.
Waziri
huyo aliyehudumu katika Serikali ya Awamu ya Nne katika wizara hiyo kwa
miaka tisa, alisema kati ya vitabu anavyoandika viwili vitatoka mwaka
huu.
“Kimoja
cha maisha yangu, ni vitabu vizuri sana, nimekuwa mwanasiasa kwa miaka
35, nimejihusisha zaidi na masuala ya utatuzi wa migogoro barani
Afrika... kitabu kingine kitahusu migogoro na Serikali za Afrika,” alisema.
Alitaja
vingine kuwa ni kuhusu uongozi na cha mwisho kitahusu siasa za Tanzania
kinachowalenga zaidi vijana kikieleza namna nchi inavyoweza kulinda
heshima yake duniani.
“Nchi
hii tumeirithi kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Yeye
alikuwa mwana ukombozi halisi. Mwaka 1963 alianzisha harakati za
ukombozi, Tanzania ikawa makao makuu ya nchi zote zinazopigania uhuru.
Vyama vya ukombozi vikaweka makao makuu yake hapa, vingine vikaanzia
harakati zake hapa,” alisema Membe.
Alisema
sifa ya kwanza ya Tanzania duniani ni ukombozi na ilikuwa mwenyekiti wa
nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi Kusini mwa Afrika.
Akizungumzia
kuhusu hatima yake kisiasa, Membe aliyewania kuteuliwa kugombea urais
kwa tiketi ya CCM kabla jina la Dk John Magufuli ambaye sasa ndiye rais
kuteuliwa, alisisitiza kuwa siasa haina mwisho.
“Tafsiri
ya siasa ni mchakato wa namna ya kuyashughulikia matatizo ya watu,
usipoyashughulikia vizuri, utaibadilisha siasa kutoka kwenye amani
kwenda kwenye mtafaruku,” alisema.
Akimnukuu
aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, Membe alisema mwanasiasa
mzuri duniani ni yule aliyeondoka kwa heshima na anayeheshimu familia
yake.
Membe
aliwataka wanasiasa walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuacha
kujipenyeza na kuendeleza ubabe wa kisiasa, akisema kufanya hivyo ni
sawa na upuuzi, badala yake wasubiri muda wao watakapochaguliwa.
VITUS MTAFYA
..... ILEJE NI NYUMBANI ......
No comments:
Post a Comment