Kiongozi
wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA Mh. Freeman
Mbowe, amesema Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu hatosafirishwa
kwenda popote mpaka pale madaktari watakaporuhusu.
Mhe.
Mbowe ameeleza hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari ikiwa
imepita siku moja tokea serikali ya Tanzania itoe kauli yake kuwa ipo
tayari kumtibia Lissu popote pale duniani kupitia Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu.
"Tundu
Lissu bado ni mgonjwa sana, hawezi kusafirishwa nje ama kutikiswa kwa
njia yeyote katika kipindi hiki kwa hiyo mpango wowote wa kumuondoa
hospitalini Nairobi kumpeleka nchi yeyote hautokuwepo kwa sasa mpaka
hapo madaktari watakaporuhusu kulingana na hali yake", amesema Mbowe.
Pamoja
na hayo, Mbowe ameendelea kwa kusema "Madaktari wametuhakikishia wana
vifaa, dawa, utaalamu wa kukamilisha awamu ya pili ya matibabu ya Mhe.
Lissu na yatafanyika hapo hapo katika hospitali ya Nairobi, Kama
kutakuwa na ulazima katika hatua za baadae basi hizo zitafanyika
kulingana na ushauri wa madaktari".
Aidha,
Mbowe amesema wamelazimika kumuwekea ulinzi mkubwa Lissu katika
hospitali aliyolazwa kutokana na kuhofia hali ya usalama iliyokuwa
imetanda juu ya Mbunge huyo kutokana na shambulio alilofanyiwa na watu
waliokosa utu.
"Nipende
kusema tunawashukuru sana uongozi wa hospitali ya Nairobi, wenzetu
walielewa hofu yetu na wametoa ulinzi wa ziada kwa ajili ya Mhe. Lissu
masaa 24 ndani na nje. Kwa hiyo Lissu yupo chini ya uangalizi mkali sana
na hili lilifanyika kutokana hofu iliyotanda na inayotanda kwa halali
kabisa kwa sababu kuna watu walitaka kuondoa maisha ya Lissu lakini
hawakuweza kufanikisha kazi yao, na hao watu hawana utu kabisa kwani
tukiwapa nafasi hawatasita kukamilisha kazi yao", amesisitiza Mbowe.
Kwa
upande mwingine, Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na
watanzania kwa ujumla kutokuwa na hofu kuhusu Mbunge wa Singida
Mashariki Tundu Lissu kwani madaktari wameshawahakikishia kuwa Lissu
atapona na kurudi kuendelea katika harakati zake alizokuwa anazifanya
kama awali.
VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......
No comments:
Post a Comment