Ajali ya Basi la Ngorika yaua askari wa JWTZ Na Kujeruhi wengine 33
Watu wawili wamefariki dunia akiwemo askari wa Jeshi la wananchi (JWTZ) na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi mali ya kampuni ya Ngorika kuigonga kwa mbele Toyota Costa eneo la Misugusugu mjini Kibaha .
Ajali
hiyo imetokea majira ya saa 1.30 asubuhi leo wakati basi hilo likitokea
Dar esalaam kwenda Arusha ambapo ilipofika eneo hilo dereva alihama
upande wake wa njia kuyapita magari mengine yaliyokua mbele yake bila
tahadhali hivyo kwenda kugongana uso kwa uso na costa iliyokua ikitokea
Miono Bagamoyo kwenda Dar esalaam.
Kamanda
wa Polisi mkoani Pwani, Jafari Mohamed amethibitisha tukio hilo na
kutaja waliokufa ni Rutta Saimon mwalimu wa shule ya msingi Mwambao
Bagamoyo na Peter Maro askari wa JWTZ na kwamba anasadikiwa kuwa ni wa
Kikosi cha Jeshi la Nyumbu Kibaha na wote walikua abiria katika Costa
hiyo.
Kamanda Jafari amesema kati ya majeruhi hao 33, wanne hali zao ni mbaya kutokana na kuvunjika sehemu mbalimbali za mwili.
"Majeruhi
wote wa ajali hiyo walipelekwa Tumbi na walitibiwa na wengi wao
wameruhusiwa kuendelea na safari yao lakini hao wanne ndiyo wamelazimika
kulazwa hapo kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya maana
wamevunjika sehemu mbalimbali za mwili, na pia miili ya marehemu
imehifadhiwa hospitalini humo kusubiri ndugu"amesema Kamanda Jafari.
No comments:
Post a Comment