Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amesema hata kama vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimefanikiwa kumwangusha kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, bado ana nguvu ya kuendelea kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na wala hajakata tamaa ya kukisuka upya chama chake.
Mrema
aliangushwa katika kiti hicho na hasimu wake kisiasa, James Mbatia,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, aliyevunja
rekodi ya kupata kura nyingi kwa upande wa wabunge wa upinzani, baada ya
kuibuka na ushindi mnono wa kura 60,187 dhidi ya 6,416 alizoambulia
Mrema (TLP) aliyekuwa akishikilia jimbo hilo huku mgombea wa CCM,
Innocent Shirima, akipata kura 16,097.
Alikuwa
akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Kilimanjaro kuhusu
majaliwa yake kisiasa, baada ya yeye na chama chake kukosa uwakilishi
kwenye Bunge na Halmashauri za Wilaya. Mbali ya kupoteza kiti cha
ubunge, TLP haikuambulia hata kiti kimoja cha udiwani.
“Chama
changu hakifi na wala sijakata tamaa, tutaanza moja na ninawaomba
wanachama wa TLP watulie…Nitashirikiana na Rais ajaye aliyetangazwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), na tutakijenga chama chetu…Hata Dk.
John Magufuli, anajua mimi ni mchapakazi na alinipigia debe na wananchi
wakapuuza,” alisema Mrema.
Katika
Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, viti saba vya
ubunge vimenyakuliwa na baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema na
NCCR-Mageuzi, huku majimbo mawili ya Mwanga na Same Magharibi,
yakiangukia CCM.
Kwa
mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na NCCR-Mageuzi
yenye mbunge mmoja mkoani Kilimanjaro, sasa zitaunda halmashauri tano
za wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo, Moshi Vijijini na
Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili za Mwanga na Same.
Majimbo hayo na idadi ya kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi zitaunda halmashauri zake ni kama ifuatavyo;
Moshi
Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati ya 21 na CCM imepata Kata mbili
za Bondeni na Kilimanjaro, wakati Jimbo la Hai, Chadema imeshinda kata
16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya Bomang’ombe ndio pekee haijafanya
uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM kufariki dunia wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu.
Aidha,
Chadema iliyoshinda kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya Rombo, ndiyo
itakayounda halmashauri ya wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi iliyoshinda
kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya udiwani katika
Jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja ya Wilaya ya
Moshi.
Katika Jimbo la Moshi Vijijini, CCM imeshinda kata moja tu.
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment