VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Monday, November 23, 2015

UVCCM Wakerwa na Tabia ya Wabunge wa UKAWA Kuwazomea Viongozi wa Kitaifa

UMOJA wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), umesikitishwa na vitendo vya  wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bungeni muda mfupi kabla ya Rais Dk. Magufuli kulifungua rasmi Bunge la 11 mwishoni mwa wiki.
Wabunge hao wa Ukawa waliwazomea baadhi ya viongozi walioongozana na Rais Dk. John Magufuli na kuamriwa  na Spika wa Bunge Job Ndugai watoke nje.
Wabunge hao wa upinznai walifanya hivyo kama hatua ya   kutokubaliana na   kufutwa   Uchaguzi wa Zanzibar na kutaka atangazwe Maalim Seif Sharif Hamad kama mshindi wa uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana   na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na kufedhehesha.
“Kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge si tabia na desturi njema… Bunge si jukwaa la vituko au maigizo bali ni eneo lenye kujenga na kuonyesha ukamilifu na ustawi wa demokrasia  na umakini wa kila mbunge na vyama vyao,” alisema Shaka.
Alisema UVCCM inaona kitendo hicho kama kielelezo cha ukomo na upeo wa hekima za wabunge ambao wameaminiwa na wananchi kuwawakilisha kwenye moja ya mihimili ya dola.
“Tukio lile ni ishara na dalili tosha  ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kuwa hawana dhamira njema ya kuijenga nchi, kupigania maendeleo ya Taifa wala kuheshimu dhamana na amana  waliyokabidhiwa na wananchi kwa njia ya demokrasia ya uchaguzi,” alisema Shaka.
Alisema ni aibu iliyovuka mipaka kwa wabunge na vyama vyao kufanya kitendo hicho huku.
Alidai kitendo hicho kinaonyesha wabunge hao kupungukiwa  ukomavu wa siasa, uwerevu, maarifa na busara za kutosha.
“UVCCM tunawaomba Watanzania kukitazama kitendo hicho na kukiona kama mwanzo wa harakati za kuzorotesha maendeleo na kasi ya mafanikio iliyopangwa na serikali ya awamu ya tano,” alisema Shaka.
Alisema wanaamini viongozi na vyombo husika vitajipanga kukabiliana nao  kuzuia aibu kama hiyo isiendelee kutokea.
UVCCM pia umempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hotuba aliyoitoa katika uzinduzi rasmi wa Bunge la  11, Dodoma.
“Hotuba ya Rais Dk. Magufuli licha ya kuwa  na umakini, matarajio, matumaini, mwelekeo, dira na  vipaumbele muhimu pia imebeba  malengo mahususi katika kuwatumikia wananchi ikiwamo kuimarisha huduma za jamii,  maendeleo ya sekta ya utawala bora, haki na demokrasia, kudumisha  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na  uhusiano wa kimataifa,” alisema Shaka.

No comments: