VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Tuesday, December 15, 2015

Wanne Wakataa Uwaziri wa Magufuli Wakihofia Kushindwa Kuendana na Kasi Yake


WABUNGE wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, wabunge wamedai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wizara 4 zilizokosa Mawaziri
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.
Kinana atoboa siri
Mwishoni mwa wiki akiwa mkoani Arusha, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alitoa siri ya wabunge wanne ambao walipigiwa simu za uteuzi wa uwaziri, lakini walikataa kwa hofu ya kushindwa kwenda na kasi ya Rais Magufuli.
Alisema anachoamini ni kwamba Rais John Magufuli, atakuwa aliwaeleza baadhi ya wabunge kuhusu nia yake ya kuwateua katika nafasi hizo, lakini wao wakamwomba asiwape majukumu hayo kwa kuwa hawana uhakika wa kwenda na kasi anayohitaji katika Serikali yake.
Kinana alisema kinachojitokeza sasa ni kama alivyoshauri Rais Magufuli kuwa si vema kwa waziri aliyeteuliwa kufanya sherehe nyumbani kwake na kuita marafiki kwa kuwa wana mzigo mzito katika kuwatumikia wananchi.
“Ni vema mawaziri hawa wakafanya maombi kwa kuwaita au kuwafuata viongozi wa dini kwani wana kazi ngumu kulingana na nia njema aliyonayo Rais Magufuli katika kupambana na masuala ya ufisadi.
“… kazi ya kupambana na ufisadi kamwe si rahisi hadi kushangilia uteuzi, lengo kubwa ni kuwaletea wananchi maendeleo kupitia ubinafsishaji wa viwanda kutoka kwa watu waliomilikishwa na kuviua,” alisema Kinana.
Katibu mkuu huyo wa CCM, alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi dunaini, hali ya kuwa wagonjwa hawana dawa.
“Nyingine ni Wiki ya Maji, mnafanya maadhimisho huku watu hawana maji, Wiki ya Maziwa wakati wafugaji wamekonda na mifugo imekonda haitoi maziwa, fedha hizo zitumike kwa mambo mengine,” alisema Kinana.

Monday, December 14, 2015

Wakulima Na Wafugaji Wauana na Kujeruhiana Morogoro......Waziri Mwigulu Afika Kutatua Ugomvi


Mkulima mmoja ameuawa, mwingine amejeruhiwa wakiwemo askari  polisi wawili kwenye mapigano dhidi ya wafugaji wa kimang’ati kwenye kijiji cha Dihimba Turiani, mkoani Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa amesema mapigano hayo yametokea baada ya wafugaji kutaka kuwachukua kwa nguvu ng’ombe zaidi ya 150 waliokuwa wakishikiliwa na wakulima kwenye ofisi ya kijiji hicho.

Mkwasa amesema siku ya tarehe 11 mwezi huu, mkulima mmoja aliyejulikana kwa jina la Bakari Mulunguza alikuta ng’ombe zaidi ya 150 wakila shambani kwake pasipo kuwa na mchungaji wa ng’ombe hao, ndipo Mulunguza alipoomba msaada kutoka kwa wakulima wenzake kwa pamoja waliwaswaga ng’ombe hao hadi kwenye ofisi ya serikali ya kijiji.

Amesema wakulima hao waliamua kuchukua uamuzi huo ili mwenye ng’ombe ajitokeze na kupigwa faini kutokana na uharibifu uliosababishwa na ng’ombe hao. Alisema siku iliyofuata ya tarehe 12, ndipo alipojitokeza mfugaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Shaabani Ikeli na kudai kuwa yeye ndiye mmiliki wa ng’ombe hao.

“Serikali ya kijiji ilimtaka mfugaji huyo kulipa faini ya Shilingi laki mbili kama fidia kutokana na uharibifu uliosababishwa ; mfugaji huyo alikubali na kuahidi kuwa angelipa faini hiyo, lakini cha kushangaza alirudi na kundi kubwa la vijana wafugaji wakitaka kuwachukua ng’ombe kwa nguvu, ndipo mapigano yalipotokea,” alisema Mkwasa.

Alimtaja aliyeuawa kuwa ni Mohamed Musa (43) mkulima wa kitongoji cha Kaole, na aliyejeruhiwa ni Charles Paulo (35) ambaye amelezwa hospitali ya Bwagala Turiani kwa matibabu.

Mkwasa amesema kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wakulima ambao walilipa kisasi kwa kuwakatakata miguu na sehemu mbalimbali za miili ng’ombe 150. Alisema polisi walifika eneo la tukio na kudhibiti vurugu hizo; amesema polisi wawili wamejeruhiwa kweye mapigano hayo.
Mwigulu Nchemba  Afika Eneo La Tukio 
Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji Mh. Mwigulu Nchemba leo hii amefika katika eneo la tukio.Akizungumza na wananchi hao Waziri  Nchemba alikuwa na haya ya kusema;

"Natoa rai kwa Wananchi hususani wa jamii ya Wafugaji na Wakulima, hakuna ardhi au mnyama mwenye thamani sawa na maisha ya mwanadamu yeyote yule,njia bora na salama ya kutatua migogoro hii inayohusisha wakulima na wafugaji ni kufuata taratibu za kuonana na uongozi wa serikali wa eneo husika hatua kwa hatua".

Pia Mh. Mwigulu amesema ameagiza ulinzi maeneo yote yenye migogoro, pili wahakikishe waliosababisha maafa wanakamatwa mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sharia na  kwa walio jeruhiwa, ameagiza wapatiwe matibabu kwanza bila kuchelewa na hatua za kisheria kwa wenye hatia zifuate.

"Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mikononi, tunakwenda kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro hii kwa kila kijiji zitakazohusisha pande zote mbili ili kubaini wavamizi wa maeneo na kuwachukulia hatua za kisheria."

 

Thursday, December 10, 2015

Breaking News: Rais Magufuli Atangaza Baraza Lake la Mawaziri

Ndugu waandishi wa habari na watanzania kwa ujumla, ninawasalimu sana. Nawakaribisha katika kikao hiki cha kutangaza baraza la mawaziri.

Tutakuwa na mawaziri 19, kuna baadhi ya wizara zitakuwa na mawaziri na hazitakuwa na manaibu waziri. Lengo ni kuwa na baraza dogo kupunguza gharama.

Zilitengwa bilioni 2, mawaziri watakapoteuliwa waende semina elekezi, baraza nitakaloliteua halitakuwa na semina elekezi na fedha tutaelekeza sehemu nyingine kama ni madawati au kwenye elimu bure.

Wizara ni 18 lakini Mawaziri ni 19 kwa sababu wizara ya Ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa Umma naiunganisha na Utawala bora hivyo itakua na mawaziri wawili. Wizara ni kama ifuatavyo;

1.Wizara ya Ofisi ya Rais,Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora.
Mawaziri - George Simbachakene  na Angella Kairuki
Naibu Waziri - Sumeilam Jafo
 
2.Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Raisi, Muungano na Mazingira
 
Waziri - January Makamba
Naibu Waziri – Luhaga Jerrson Mpina

3.Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu
 
Waziri - Jenista Muhagama
MaNaibu – Dkt. Possy Abdallah na Anthony Mavunde.

4.Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
 
Waziri - Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri - William Ole Nasha

5.Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 
Waziri : Bado hajapatikana.
Naibu Waziri – Inj. Edwin Ambandusi Ngonyani

6.Wizara ya Fedha na Mipango
 
Waziri: Bado hajapatikana.
Naibu Waziri - Ashantu Kizachi

7.Wizara ya Nishati na Madini
 
Waziri - Prof. Mwigalumi Muhongo.
Naibu Waziri - Medalled Karemaligo.

8.Wizara ya Katiba na Sheria,
Waziri - Harrison Mwakyembe

9.Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
 
Waziri - Dk. Augustino Mahiga
Naibu Waziri – Dkt. Susan Kolimba.

10.Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Waziri - Dk. Hussein Mwinyi

11. Wizara ya Mambo ya Ndani
Waziri - Charles Kitwanga.

12.Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 
Waziri - William Lukuvi
Naibu Waziri - Angelina Mabula

13. Wizara ya Maliasili na Utalii
Waziri: Bado hajapatikana.
Naibu Waziri– Inj. Ramol Makani

14: Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
 
Waziri: Charles Mwijage.

15: Wizara ya Elimu,Sayansi Teknolojia na Ufundi.
 
Waziri: Bado hajapatikana.
Naibu Waziri – Inj. Stella Manyanya

16: Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
 
Waziri - Ummy Mwalim
Naibu Waziri –  Dkt. Hamis Kigwangala

17: Wizara ya Habari, Utamadu, Wasanii na Michezo
 
Waziri - Nape Nnauye
Naibu Waziri - Anastasia Wambura.

18:Wizara ya Maji na Umwagiliaji
 
Waziri – Prof. Makame Mbarawa
Naibu  Waziri– Inj. Isack Kamwela

Monday, December 7, 2015

NEC Yatoa Tamko Kuhusu Uchaguzi Wa Wabunge Arusha Mjini Na Handeni.

Na Jacquiline Mrisho-Maelezo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza siku ya kupiga kura kwa baadhi ya majimbo ambayo uchaguzi wake ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali
 
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametaja siku hiyo ya uchaguzi itakuwa Disemba 13, mwaka huu.

“Natoa rai kwa Wananchi wote waliojiandikisha kama wapiga kura katika Majimbo na Kata husika kujitokeza katika vituo walivyojiandikishia ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka” amesema Lubuva.

Jaji Lubuva aliyataja majimbo hayo ambayo wananchi watapiga kura za kuchagua Wabunge kuwa ni Majimbo ya Arusha Mjini na Handeni Mjini ambapo uchaguzi wa Madiwani katika kata  za Mvomero, Ipala na Nyamwilolewa nao utafanyika siku hiyo.

Aidha, Jaji Lubuva  amesisitiza kuwa, taratibu zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 mwaka ndizo zitakazotumika kwenye uchaguzi kwenye majimbo hayo na kata hizo.

Kwa ufupi, Jaji Lubuva alikumbushia baadhi ya taratibu hizo zikiwemo za mpiga kura kubeba kadi yake ya kupigia kura pindi aendapo kupiga kura, mawakala wa vyama vya siasa lazima wawepo kwenye kila kituo na pia Maafisa Uchaguzi  kufungua kituo na kufunga kwa muda uliopangwa na Tume.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, uchaguzi wa Wabunge na Madiwani wa Majimbo 7 pamoja na Kata 35  ulihairishwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vifo na vurugu.

Thursday, December 3, 2015

Rais Dkt. Magufuli atoa siku saba kwa wafanyabiashara wakwepa kodi.



Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt.John  Pombe  Magufuli amewapa siku saba kuanzia tarehe 03/12/2015 wafanyabiashara wote ambao waliingiza mizigo yao bila kulipa kodi wakalipe kwani baada ya hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria
 
Hayo  yamesemwa leo Ikulu  jijini Dar es Salaam na Mheshimiwa Rais katika mkutano wake na wadau wa sekta binafsi  alipoamua kufanya mazungumzo nao pamoja na kuwasikiliza maoni  yao ikiwa ni sehemu ya ahadi zake katika kipindi cha kampeni za kuomba kura za kiti cha Urais,lengo likiwa ni kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Rais  aliendelea kusema kuwa katika kipindi hichi cha miaka mitano amedhamiria kuijenga nchi na watu wasimuelewe vibaya kwa maamuzi anayofanya kwani ni kwania njema ya kuleta maendeleo na siyo ujeuri.

“Tutaangalia namna ya kupunguza utitiri wa ushuru katika bidhaa mbalimbali,mfano katika kipindi cha kampeni niligundua katika Mkoa wa Kagera na Kilimanjaro wanakolima zao la Kahawa,wamekuwa wakitozwa tozo  26 kwa zao hilo na hiyo imechangia kusababisha wafanyabiashara wa zao hilo kufanya biashara haramu ya kupeleka zao hilo kwa magendo kuuza  katika nchi jirani”,alisema Mheshiwa Rais Dkt. Magufuli.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Dkt.Magufuli amewaahidi wadau wasekta binafsi ushirikiano mkubwa kwani anatambua mchango wao katika kukuza uchumi na pia amewataka wadau hao kuwa wazalendo na kuliacha kukwepa kulipa kodi ili tuweze kujenga taifa lenye maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli  ameendelea kusema kuwa kama kutakuwa na mfayabiashara yeyote  atakayetaka kuwekeza  na akakwamishwa na  mtu aliyechini ya uteuzi wake  basi mtu huyo ataondoka kwani sasa ni wakati wa wadau wa sekta binafsi kuanza kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyo toa ajira.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amewapa mawazo ya kibiashara wadau wa sekta binafsi kuanzisha kampuni ya kutenganisha udongo unaotoka kwenye machimbo ya madini,kuanzisha viwanda vya samaki pembezoni mwa bahari pamoja na kutengeneza samani zitokanazo  na mazao ya misitu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw.Regnald Mengi amesema kuwa wako tayari kumpa ushirikiano mkubwa  Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha uchumi watanzania unakuwa kwa haraka na pia amemuomba mheshimiwa rais kuendelea kukemea masuala ya rushwa  pamoja kusaidia kupunguza utitiri wa kodi

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Reginald Mengi akiongea katika mkutano huo na kumuahidi Rais Dkt. Magufuli ushirikiano katika kutekeleza yale anayodhamiria kwenye serikali yake ikiwemo kusimamia ulipaji kodi kwa dhumuni la kuiinua Tanzania kiuchumi
 

Baadhi ya Wadau wa Sekta Binafsi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mkutano huo Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
 

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Reginald Mengi akimpongeza  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipomaliza kutoa hotuba kwa wajumbe wa Sekta Binafsi nchini Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimueleza Jambo Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Reginald Mengi wakati wa Mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi nchini Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.

Monday, November 23, 2015

UVCCM Wakerwa na Tabia ya Wabunge wa UKAWA Kuwazomea Viongozi wa Kitaifa

UMOJA wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), umesikitishwa na vitendo vya  wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bungeni muda mfupi kabla ya Rais Dk. Magufuli kulifungua rasmi Bunge la 11 mwishoni mwa wiki.
Wabunge hao wa Ukawa waliwazomea baadhi ya viongozi walioongozana na Rais Dk. John Magufuli na kuamriwa  na Spika wa Bunge Job Ndugai watoke nje.
Wabunge hao wa upinznai walifanya hivyo kama hatua ya   kutokubaliana na   kufutwa   Uchaguzi wa Zanzibar na kutaka atangazwe Maalim Seif Sharif Hamad kama mshindi wa uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana   na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na kufedhehesha.
“Kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge si tabia na desturi njema… Bunge si jukwaa la vituko au maigizo bali ni eneo lenye kujenga na kuonyesha ukamilifu na ustawi wa demokrasia  na umakini wa kila mbunge na vyama vyao,” alisema Shaka.
Alisema UVCCM inaona kitendo hicho kama kielelezo cha ukomo na upeo wa hekima za wabunge ambao wameaminiwa na wananchi kuwawakilisha kwenye moja ya mihimili ya dola.
“Tukio lile ni ishara na dalili tosha  ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kuwa hawana dhamira njema ya kuijenga nchi, kupigania maendeleo ya Taifa wala kuheshimu dhamana na amana  waliyokabidhiwa na wananchi kwa njia ya demokrasia ya uchaguzi,” alisema Shaka.
Alisema ni aibu iliyovuka mipaka kwa wabunge na vyama vyao kufanya kitendo hicho huku.
Alidai kitendo hicho kinaonyesha wabunge hao kupungukiwa  ukomavu wa siasa, uwerevu, maarifa na busara za kutosha.
“UVCCM tunawaomba Watanzania kukitazama kitendo hicho na kukiona kama mwanzo wa harakati za kuzorotesha maendeleo na kasi ya mafanikio iliyopangwa na serikali ya awamu ya tano,” alisema Shaka.
Alisema wanaamini viongozi na vyombo husika vitajipanga kukabiliana nao  kuzuia aibu kama hiyo isiendelee kutokea.
UVCCM pia umempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hotuba aliyoitoa katika uzinduzi rasmi wa Bunge la  11, Dodoma.
“Hotuba ya Rais Dk. Magufuli licha ya kuwa  na umakini, matarajio, matumaini, mwelekeo, dira na  vipaumbele muhimu pia imebeba  malengo mahususi katika kuwatumikia wananchi ikiwamo kuimarisha huduma za jamii,  maendeleo ya sekta ya utawala bora, haki na demokrasia, kudumisha  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na  uhusiano wa kimataifa,” alisema Shaka.

Monday, November 2, 2015

MREMA Afunguka: Sijakata Tamaa, Nitaendelea Kuwania Nafasi Mbalimbali za Kisiasa


Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amesema hata kama vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimefanikiwa kumwangusha kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, bado ana nguvu ya kuendelea kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na wala hajakata tamaa ya kukisuka upya chama chake.

Mrema aliangushwa katika kiti hicho na hasimu wake kisiasa, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, aliyevunja rekodi ya kupata kura nyingi kwa upande wa wabunge wa upinzani, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa  kura 60,187 dhidi ya 6,416 alizoambulia Mrema (TLP) aliyekuwa akishikilia jimbo hilo huku mgombea wa CCM, Innocent Shirima, akipata kura 16,097.

Alikuwa akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Kilimanjaro kuhusu majaliwa yake kisiasa, baada ya yeye na chama chake kukosa uwakilishi kwenye Bunge na Halmashauri za Wilaya. Mbali ya kupoteza kiti cha ubunge, TLP haikuambulia   hata kiti kimoja cha udiwani.

“Chama changu hakifi na wala sijakata tamaa, tutaanza moja na ninawaomba wanachama wa TLP watulie…Nitashirikiana na Rais ajaye aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), na tutakijenga chama chetu…Hata Dk. John Magufuli, anajua mimi ni mchapakazi na alinipigia debe na wananchi wakapuuza,” alisema Mrema.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, viti saba vya ubunge vimenyakuliwa na baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema na NCCR-Mageuzi, huku majimbo mawili ya Mwanga na Same Magharibi, yakiangukia CCM.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na NCCR-Mageuzi yenye mbunge mmoja mkoani  Kilimanjaro, sasa zitaunda halmashauri tano za wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo, Moshi Vijijini na Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili za Mwanga na Same.

Majimbo hayo na idadi ya kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi zitaunda halmashauri zake ni kama ifuatavyo;
Moshi Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati ya 21 na CCM imepata Kata mbili za Bondeni na Kilimanjaro, wakati Jimbo la Hai, Chadema imeshinda kata 16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya Bomang’ombe ndio pekee haijafanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM kufariki dunia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Aidha, Chadema iliyoshinda kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya Rombo, ndiyo itakayounda halmashauri ya wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi iliyoshinda kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya udiwani katika Jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja ya Wilaya ya Moshi.

Katika Jimbo la Moshi Vijijini, CCM imeshinda kata moja tu.
Mpekuzi blog