Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia vijana watano
wa kundi la wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa tuhuma za
kufanya uchochezi na kufanya mikusanyiko isiyo halali jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova alisema vijana hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti
kwa makosa ya kuunda kikundi kisicho halali kwa mujibu wa sheria za
nchi na kuwahamasisha wenzao, kuandamana hadi Ikulu kwa Rais Jakaya
Kikwete kudai ajira za kudumu.
“Tunawashikilia
vijana watano ambao ndio viongozi wa kikundi kinachojiita umoja wa
wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Mwenyekiti ndio alikuwa wa kwanza
kukamatwa na wengine tuliwakamata juzi mara baada ya kukusanyika eneo la
Msimbazi Centre na Muhimbili,” alisema Kova.
Akieleza
chanzo cha vijana hao kutaka kuandamana kuelekea Ikulu, alidai wahitimu
hao wanadai kuahidiwa ajira za kudumu walipomaliza mafunzo yao na hivyo
baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuajiriwa, ndipo wakaamua kuanzisha
kikundi hicho ili kwenda kumwona Rais Kikwete kumweleza tatizo la ajira
linalowakabili.
“Vijana hawa wanadai kuwa waliahidiwa kupewa ajira za kudumu mara baada ya kumaliza mafunzo yao ya JKT.
"
Jambo hili sio la kweli, kwani tumefanya uchunguzi na kubaini hakuna
mkataba wowote unaosema wakimaliza mafunzo lazima waajiriwe, bali kila
mtu anatakiwa kutumia ujuzi alioupata kujiajiri.
"Lakini
walipokaa kwa muda mrefu bila kuona ahadi yao inatekelezwa, wakaamua
kuanzisha kikundi chao ambacho sio halali kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Hadi
sasa tumeandaa jalada la mashitaka na tumelikabidhi kwa mwanasheria wa
serikali kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hawa kujibu
mashitaka yanayowakabili,” aliongeza Kova katika taarifa yake.
Alitaja
vijana wanaoshikiliwa na Polisi kuwa ni Mwenyekiti wa kikundi hicho
George Mgoba (28) mkazi wa Mabibo Loyola, Katibu wao Linus Emmanuel (28)
mkazi wa Tabata, Emmanuel Richard (28) mkazi wa Kawe, Jacob Joseph (36)
mkazi wa Mabibo na Rizione Ngowi (27) mkazi wa Mtoni Mtongani.
Akizungumzia
tuhuma za kutekwa na kuteswa kwa George Mgoba, Kova alisema Jeshi la
Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini tukio hilo kama ni la kweli
na kwanini watu hao walimteka.
“Tunaendelea
na uchunguzi kubaini kama ni kweli kijana huyo alitekwa kama anavyodai
kuwa Februari 16 alitekwa na kupatikana tarehe 19 majira ya saa nne
usiku huko Tungi Kibaha kandokando ya barabara, pia tujue ni akina nani
walimteka na kwasababu zipi kisha watu hao tutawapeleka mahakamani,” alisema Kova.
Kova alieleza kuwa “Februari
22 mwaka huu majira ya saa kumi na moja jioni, George Mgoba alijaribu
kutoroka wadini katika Hospitali ya Muhimbili lakini polisi walibaini
ujanja wake na kufanikiwa kumweka kizuizini. Lengo lake ilikuwa ni
kukimbia matibabu na kuzua hofu kwa wananchi”.
Kwa sasa Mwenyekiti huyo wa vijana hao bado amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akipatiwa matibabu.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja katika
Hospitali hiyo ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hali
ya mtu huyo, inaendelea vizuri na afya yake imeimarika.
Wakati
huo huo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baadaye jana, Kova
alimtaka Makamu Mwenyekiti wa Vijana hao, Parali Kiwango (25) mkazi wa
Temeke Mikoroshini ajisalimishe mara moja Polisi kwa ajili ya mahojiano
zaidi, kabla jeshi hilo halijaanza kumtafuta.
“Jeshi
la Polisi linamtaka Makamu Mwenyekiti ajisalimishe mara moja kwani jana
alipoona Katibu wake amekamatwa alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
"Yeye
kama ni mhitimu wa JKT hatakiwi kukimbia, bali ajisalimishe mwenyewe
katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam au
kituo chochote cha Polisi kilicho karibu na alipo,” aliongeza Kova.