MADIWANI wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Vijijini, wamefikia makubaliano ya pamoja
kumwondoa kwenye nafasi yake afisa elimu shule za Msingi wa wilaya hiyo, Dionis
Boay, kutokana na Halmashauri hiyo kushika nafasi ya mwisho katika matokeo ya
darasa la saba.
Maazimio
hayo yalifikiwa jana katika kikao cha Baraza la madiwani, kilichofanyika katika
ukumbi wa Halmshauri hiyo.
Pamoja na
mijadala mingine, lilipofika suala la elimu, Afisa elimu huyo alisimama na
kuwasilisha taarifa ya elimu na jinsi idara yake inavyojipanga kufuta aibu ya
kushuka kwa ufaulu katika wilaya hiyo, ndipo diwani wa kata ya Masoko, Edward
Mwampamba(Chadema), aliposimama na kusema kuwa chanzo cha matokeo mabaya katika
wilaya hiyo ni maafisa elimu.
(Maafisa
elimu ndiyo chanzo cha ufaulu mbaya katika wilaya yetu, hususani katika kata
yangu, kuna walimu saba wamehamishwa na hawataki kuleta walimu wengine” alisema
Mwampamba na kuwataja majina walimu hao.
Diwani wa
kata ya Ilungu, Hashim Mwashang’ombe, alisema kuwa kutokana na Halmashauri hiyo
kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, anahitaji afisa
elimu na jopo lake la taaluma ngazi ya wilaya wapishe ofisi hizo kuanzia jana.
Akiwa anaendelea
kuwashawishi madiwani wenzake kukubaliana na hoja yake, ndipo Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo, Andason Kabenga, alipochukua kipaza sauti na kusema kuwa
jambo hilo halipaswi kuchukuliwa mzaha na kupoteza muda kulijadili bali Afisa
elimu huyo na timu yake wanapaswa kuondolewa haraka.
“Sioni kuwa
hili ni jambo la kujadili kwa muda mrefu, bali afisa elimu anapaswa kuondolewa
kwenye nafasi hiyo na wenzake” alisema Kabenga huku madiwani wakipiga makofi na
kwamba hawawezi kuendelea kucheka na nyani.
Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya, Upendo Sanga.(Picha na maktaba)
Baada ya
maazimia hayo ya madiwani kuhusu afisa elimu huyo na jopo lake ngazi ya wilaya,
ndipo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Upendo Sanga, aliposoma sheria na kuomba
waalikwa kuwapisha madiwani na kugeuza Baraza hilo kuwa kikao.
Mbali na
jambo hilo, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Mch. Luckson Mwanjale, alibanwa
na baadhi ya madiwani kuwa aeleze kwanini anatoa ahadi kwa wananchi na
kuzitumia fedha za mfuko wa jimbo bila kukaa kwanza na kamati ya fedha.
Akitoa majibu
ya swali hilo, Mbunge huyo alisema kuwa, sheria za matumizi ya mfuko wa jimbo
zipo wazi ikiwemo kuwaambia wananchi kupeleka barua ofisini kwake kabla ya
kuwaahidi kutatua shida za maendeleo au kuwaahidi hata kabla ya barua na kufika
katika kamati ya fedha.
No comments:
Post a Comment