KATIBU wa vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokuwa wakiandamana kushinikiza Serikali kuwapatia ajira, Rinus Emmanuel amekamatwa jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wao George Mgoba,
kutekwa wiki iliyopita na kisha kupigwa na kuteswa na watu
wasiojulikana.
Hata hivyo Mgoba alihamishwa kutoka Hospitali ya Amana, Ilala na
kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambapo anaendelea
kupata mateso kutokana na kutopatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Katibu huyo alikamatwa jana akiwa na wenzake wawili wakati wakiwaongoza
wenzao kwenda kumwona mwenyekiti wao, aliyelazwa katika Hospitali ya
Muhimbili.
Akizungumza na Mpekuzi jana, Msemaji wa vijana hao, Omary Bakari
alisema katibu wao alichukuliwa ghafla na polisi walipokuwa wanaingia
eneo la Muhimbili muda mchache baada ya kushuka kwenye gari.
“Hatujui nini kinaendelea hadi sasa na kwa nini polisi wanatufanyia
vitendo hivi wakijua sisi si wahalifu, tunasikitika sana kwa haya
yanayoendelea kufanyika juu yetu,” alisema Bakari.
Alisema pamoja na kukamatawa kwa katibu wao na watu waliodai ni askari
polisi wamefuatilia kwa vyombo vinavyohusika ikiwemo polisi lakini
wamekuwa wakipewa majibu ya kukatisha tama, jambo ambalo linawafanya
waingiwe na hofu kuhusu hatima ya kiongozi wao.
Zaidi ya vijana 300 walikuwa wakiingia hopitalini hapo , huku baadhi yao
wakiwa nyuma ghafla walishuka askari wakiwa wamevaa kiraia ambao
walimvamia katibu wao na kuingia nae katika gari na kutokomea naye
kusikojulina.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa vijana hao, Kiwango Mpalare, alisema
kabla ya kwenda Muhimbili walikuwa na kikao chao katika Ukumbi wa
Msimbazi Centre ambapo pamoja na mambo mengine walijadili hatima ya
kumuuguza kiongozi wao.
“Baada ya kikao wote tulitoka na kuazimia kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili kwa lengo la kumjulia hali kiongozi wetu.
“Baada ya kufika hospitali tukiwa zaidi ya vijana 300 walikuja askari
wakiwa katika gari na kumkamata katibu wetu kwa kosa la kukusanyika
kinyume cha sheria. Tunajiuliza wapi tumekusanyika hali ya kuwa tulikuwa
kwenye ukumbi wa mikutano.
“… je hata katika ukumbi wa mikutano napo kunahitajika kibali cha
polisi, baada ya taarifa hiyo tulifuatilia polisi na kuambiwa kuwa
waende wanasheria kwa ajili ya dhamana. Lakini ilishindika na wote wapo
Kituo cha Polisi Cetral,” alisema Maparale.
Mwandishi alipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kiliposi Ilala, Mary
Nzuki ili kupata ufafanuzi kuhusu kukamatwa kwa vijana hao alipokea simu
na alipoulizwa swali aliikata.
Hata alipopigiwa kwa mara nyingine zaidi ya mara tatu simu yake iliita bila kupokelewa.
Kutokana na tukio hilo alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salam, Kamishna Suleiman Kova, alisema bado hajapata taarifa za
kukamatwa kwa vijana hao ambapo aliomba afanye uchunguzi wa kina na
taarifa atatoa leo.
Wiki iliyopita kiongozi wa vijana hao, Mgoba alitekwa na kisha kuteswa
na watu ambao hawajajulikana, alihamishiwa katika Hospitali ya Muhimbili
Ijumaa jioni akitokea Hospitali ya Amana alikokuwa amelazwa awali.
Mwenyekiti wa JKT, George Mgoba akiwa wodini.
Baadhi ya askari wa JKT wakiwasili Muhimbili.
Askari Wakiimarisha Ulinzi eneo la Hospitali ya Muhimbili
No comments:
Post a Comment