SIASA za
mkoa wa Mbeya, zina historia kubwa sana. Historia hiyo haimwachi mbali,
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya kwa miaka 15, Patrick Nswilla, John
Mwakangale, mzee Mwambulukutu na Waziri asiye na wizara maalum ofisi ya Rais,
Prof. Mark James Mwandosya.
Kiongozi
huyu ni Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki, lililopo katika Halmashauri ya
Busokelo mkoani hapa.
Kwa mkoa wa
Mbeya kwa wanasiasa waliopo ndani ya mfumo wa siasa za mkoa huu, yeye ndiye
mwanasiasa anayeheshimika zaidi kutokana na hulka yake ya kutabasamu na watu wa
rika zote na hasa kuwa mmoja ya viongozi ambao walianza kuthubutu kuwania
nafasi ya rais mwaka 2005.
Baadhi ya
wananchi wa mkoa wa huu, wanamwita Prof. Mwandosya Baba wa siasa za mkoa wa Mbeya.
Heshima hiyo
inatokana na yeye kuwa kiongozi wa NEC mkoa wa Mbeya, ambao aliupata baada ya
mchuano mkali kati yake na Kijana Thom Mwang’onda mwaka 1997, kisha kuibuka mshindi.
Akawa kiongozi
mwenye heshima kubwa kwa siasa za Mkoa wa Mbeya, kabla hajakengeuka na
kujisahau kutohudhuria vikao vya chama chake, mkoa wa Mbeya.
Wakati baadhi
wakiendelea kumpa heshima yake, baadhi ya waliokuwa wapambe wake mwaka huo,
hawataki hata kumsikia kutokana na madai kuwa baada ya uchaguzi kuisha hakuweza
kuwakumbuka hata kwa salaam na wakawa wanabezwa na kundi la Thom Mwang’onda.
Mmoja ya
wapambe wa Prof. Mwandosya anayesikika mara kadhaa na kudai kuwa hajawahi
kuthaminiwa baada ya ushindi ni aliyekuwa diwani wa kata ya Utengule Usongwe,
Mwalimu Jackob Mwakasole, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Kanisa la
Uinjilisti Tanzania, lenye makao makuu mjini Mbalizi, wilaya ya Mbeya.
Mwingine ambaye
licha ya kumkataa kwa muda mrefu, lakini kwa sasa analitangaza vema jina la
Prof. Mwandosya na kuamini kuwa akiteuliwa kuwania nafasi ya Rais kupitia CCM, atakuwa kiongozi bora, ni Katibu Mwenezi wa
CCM Mkoa wa Mbeya, Bashiu Madodi.
Kwa wafuatiliaji
wa masuala ya siasa kwa mkoa wa Mbeya, Prof. Mwandosya anaendelea kukumbukwa
kwa umahili wake wa kusimamia na kuhakikisha miradi kadhaa inakamilika bila
upendeleo, bali kwa kufuata taratibu za serikali.
Anakumbukwa kwa
kusimamia kidete uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe ambao umekamilika
katika wilaya ya Mbeya, Jimbo la Mbeya Vijijini.
Inaelezwa kuwa,
asingekuwa Mwandosya uwanja huo wa ndege ungeenda kujengwa mikoa ya Kaskazini,
ingawa haikuwa dhamira ya serikali.
Mbali na
uwanja huo wa kimataifa, pia anaendelea kukumbukwa kupigania adhima ya serikali
kukifanya chuo cha ufundi MIST kuwa chuo kikuu cha Sayansi na teknolojia(MUST),
kilichopo Iyunga Jijini Mbeya.
Sanjari na
miradi hiyo mikuu miwili, pia mradi mkubwa wa maji, ambao ulizinduliwa Julai,2012
na Rais Jakaya Kikwete, jina la uongozi uliotukuka wa Prof. Mark Mwandosya,
linasadifu.
Prof.
Mwandosya ni mmoja kati ya viongozi ambao wanatajwa kuwania nafasi ya rais
mwaka huu, kupitia chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Jakaya
Kikwete, anao mtihani mkubwa katika uteuzi kama kweli ataangalia suala la
urafiki. Edward Lowassa rafiki yake, Benard Membe rafiki yake, January Makamba
kijana wake, Mwigulu Nchemba kijana wake, Mizengo Pinda rafiki yake na Prof.
Mwandosya ni rafiki yake.
Ni mara
chache ambazo Rais Kikwete amefanya ziara mkoani Mbeya bila kuambatana na Prof.
Mark Mwandosya na hata katika matembezi ya sherehe za miaka 37 za CCM
zilizofanyika mwaka jana 2014, mkoani Mbeya, alikuwa na Prof. Mwandosya na
kiongozi huyo aliutangazia umma kuwa kwa sasa amepona na anamshukuru sana Rais
Kikwete kwa kumtibu.
Kauli hiyo,
ilihisiwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa ni salamu tosha kwa wawania
nafasi ya rais mwaka huu 2015, ukizingatia kuwa kiongozi huyo alishika nafasi
ya tatu mwaka 2005 katika mbio hizo za urais, ambapo kambi yae kubwa ilikuwa
kanda ya Ziwa na sasa kambi yake imeongezeka katika kanda ya Nyanda za juu
kusini.
Mbali na
mapungufu ya Mwandosya kwa wanasiasa wa mkoa wa Mbeya, hasa yanayotokana na
hasira za baadhi ya wapambe wake wa mwaka 1997 kwenye nafasi ya NEC, kiongozi
huyu anaonekana kurejesha imani kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya wajumbe wa
Halmashuri kuu ya Taifa waliopo mkoani Mbeya na Nyanda za juu kusini.
Wajumbe hao,
awali baadhi yao walikuwa wakijinasibu kuwa ni wapiga kura watiifu wa aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, lakini wamebadili msimamo baada ya kile wanachodai
kuwa wanaridhishwa na propaganda za kwamba wapambe wa Lowassa, wanawatembelea
baadhi ya watu huku wao wakiwa wanatengwa, hivyo kuona kama kambi hiyo imejaa
matapeli na hivyo ni bora kuwa wapiga kura huru.
Baadhi ya
wajumbe hao, wanasema kuwa, nafasi za kura walizonazo ni tatu, hivyo moja ya
kura zao itaangukia kwa Prof. Mwandosya kati ya majina matano ambayo
yatapelekwa kwenye kikao chao na kamati kuu.
Baadhi ya
watanzania hofu yao ni kwamba, dunia kwa sasa inapigana kuhusu suala la uchumi,
je nani kati ya waliojitokeza anaweza kumudu kusimamia rasilimali za Tanzania
kwa uadilifu na kukataa kuwa kibaraka wa ‘’viranja’’ wa dunia? Je ni Prof. Mark
Mwandosya ataweza kutimiza adhima ya watanzania au kuendelea kuwaunganisha
wananchi wa Mbeya?
Nawaasa viongozi
wa CCM hasa wale wenye kura za maamuzi, kuwaletea watanzania mgombea anayeweza
kuangalia uchumi wa dunia unakoelekea na namna mataifa yanavyochukua umiliki wa
uendeshaji wa shughuli muhimu za kiuchumi kisha ajiulize kuwa je hii si sehemu
ama aina mpya ya ujamaa?
Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere angekuwepo leo hii angesemaje? Hakuna mwenye jibu
sahii lakini kwa kuwa alishaonya kwenye hotuba zake, ninaloweza kuhisi ni kuwa
angekumbusha kile alichowahi kusema, ambacho wengi hawakudhani kuwa kingetimia
na ungekuwa wakati wa kudhihirika tena kwa maono yake.
na makala haya inapatikana katika gazeti la MTANZANIA TAREHE 18/01/2015