Walimu Jiji la Mbeya, wakiwa wamezuiwa na FFU ili wasiendelee kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya.
WALIMU
wa shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya,
wapatao 113, juzi waliandamana kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji hilo
kwa ajili ya kudai haki zao mbalimbali.
Maandamano
hayo ya amani, yalianzia katika ofisi kuu ya Jengo la CWT Mkoa wa Mbeya
majira ya saa 5;27 asubuhi, kabla hayajazuiwa na kikosi cha askari wa
kutuliza ghasia mkoani hapa saa 5;33 mpaka saa 5;39 na kuwaomba warejee
ofisini kwao kutokana na hali ya vurugu iliyokuwa imelizingira Jiji hilo
jana.
“Tunawaomba mrudi ofisini kwenu na sisi
tutaenda kumleta Mkurugenzi wa Jiji, kwasababu hata mkijaribu kwenda
muda huu hamtaweza kuonana naye, ulinzi umeimarishwa sana kutokana na
mgomo wa wafanyabiashara wa soko la Soweto ambao wamegoma na wanataka
kuandamana” alisikika mmoja wa askari mwenye nyota tatu, akiwasihi
walimu hao.
Wakizungumza na waandishi wa
habari, walimu hao walisema kuwa, walifikia uamuzi wa kwenda kumuona
mwajiri wao kutokana na madai mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya
mishahara yao tangu mwaka 2007.
“Mwalimu
unaingia darasani ukiwa na mawazo ya fedha zako huku ukiangalia dawati
la mwanafunzi limechoka. Serikali inajisikia raha kuona mwalimu anaenda
na biashara ya ubuyu shuleni! Mimi nadai zaidi ya Milioni Nne tangu
mwaka 2007 sijalipwa na fedha tunaambiwa zimekuja zinafanya kazi
zingine”alisema Mwalimu Stella Robson.
Mwalimu
Lucas Mahenge, ambaye ni mlemavu wa macho, alisema kuwa yeye madai yake
ni suala la kupandishwa madaraja bila kupandishwa mshahara, hali ambayo
alisema inamkatisha tamaa na serikali isifikie mahala ikawafikirisha
walimu kuanza kuwafundisha watoto kuwa 2+2=22.
“Serikali
kama imeshindwa kutulipa madai yetu, ituambie ili tuweze kumwomba
mfanyabiashara, Rwegemalil” alisema Mwalimu Gunza Mwasomola.
Katibu
wa Chama cha walimu Jiji la Mbeya, Mwalimu Felix Mnyanyi, alisema kuwa
kwa kushirikiana na viongozi wenzake, wamefuatilia kwa muda mrefu madai
hayo na kufanya uhakiki lakini utekelezaji wake umekuwa siyo wa
kuridhisha.
“Walimu wamefika hapa wakiwa na
madai zaidi ya matatu, ambayo ni malimbikizo ya mishahara tangu mwaka
2007, ambapo ni wilaya pekee nchini walimu hawajalipwa, madai ya fedha
za likizo, kupanda na kushushwa madaraja baada ya kujiendeleza kitaaluma
na walimu wastaafu kutolipwa” alisema Mwalimu Mnyanyi.
Alisema
kuwa baada ya kuzuiwa na kuwaelewa askari polisi kuwa wasifike katika
ofisi ya mwajiri wao ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, kutokana na
hali ilivyokuwa ya utata wa usalama wao na watu wengine, walirejea
ofisini hapo na kuendelea kumsubiri mwajiri huyo chini ya ulinzi wa
polisi, hali ambayo mpaka majira ya saa saba mchana, walimu waliendelea
kuwepo katika ofisi yao na Mkurugenzi hakuweza kufika kwa wakati huo
mpaka tunaenda mitamboni.
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya,
Mussa Zungiza, alikiri kuwepo madai ya walimu katika ofisi yake na
kwamba madeni hayo hayatawezwa kumalizwa kwa siku moja kutokana na
walimu kutofautiana muda wa kuanza likizo na kumaliza.
Alwaambia walimu kuwa atashughulikia madai yao kwa kushirikiana na uongozi wao wa CWT.
No comments:
Post a Comment