Mtaalamu wa Masuala
ya Forodha kutoka TRA, Bw. Stambuli Myovela (Kulia) akizungumza wakati wa Semina
ya Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) kwa watumishi wa Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango.
Baadhi ya watumishi
wataalamu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia kwa umakini
mawasilisho kuhusu Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) katika
semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Mfumo wa Himaya
Moja ya forodha uliridhiwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki
katika Mkutano wake wa 28 ambapo kwa pamoja Mawaziri hao waliridhia kuwa na Mpangokazi
unaoainisha masuala ya kutekeleza katika kipindi cha miezi sita ili kuwezesha
kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Forodha ifikapo mweizi Juni, 2014.
Na Saidi Mkabakuli
Mamlaka ya Mapato nchini
(TRA) imetoa semina juu ya Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory)
kwa watumishi na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Akizungumza katika ufunguzi
wa Semina hiyo, Naibu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango na Mkuu
wa Kongane ya Biashara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kiuchumi, Bw. Paul Sangawe
amesema kuwa semina hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kuna uelewa wa pamoja
kuhusu utaratibu huo kwa watumishi wa umma na watanzania wote.
“Lengo la semina hii ni
kupata ufahamu wa kutosha kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea, ili kuweza
kushauri Serikali ipasavyo katika masuala mbalimbali ya kisera katika
Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,” alisema Bw. Sangawe.
Akiwasilisha mada
juu ya Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha kwa watumishi, Mtaalamu wa Masuala ya
Forodha, Bw. Stambuli Myovela alisema kwamba mfumo huo unaainisha utaratibu wa
Mzunguko Huru wa Biashara, Usimamizi wa Mapato, na Mfumo wa Kisheria.
Bw. Myovela
aliongeza kuwa kwa mujibu ya mfumo uliokubalika ni kwa kila Nchi Wanachama
zitakushanya mapato yake ya kodi. Aidha, kwa bidhaa zinazopitia Nchi moja
kuelekea katika Nchi nyingine wanachama (Transit Goods), Nchi Wanachama zimekubaliana
kuwa nchi husika bidhaa zinapokwenda itakusanya mapato yake na kuifahamisha
mamlaka ya forodha mizigo ilipoingilia katika Jumuiya kwa ajili ya kuruhusu
bidhaa kuondoshwa.
Akieleza namna
ya utendaji kazi wa mfumo huo, Bw. Myovela aliongeza: “Baada ya kuthibitisha
kuwa kodi imelipwa, mizigo itasafirishwa kutoka kituo cha kwanza cha forodha
chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Forodha kwenda nchi ambayo mizigo hiyo imekusudiwa
kutumika ndani ya Jumuiya. Mfumo maalum wa ufuatiliaji kielektroniki (Electronic
Cargo Tracking System) utatumika kuhakikisha mizigo inafika salama katika nchi
iliyokusudiwa katika Jumuiya.”
No comments:
Post a Comment