Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kitaitisha maandamano kwenye mikoa yenye gesi ili kulishinikiza Bunge kupinga muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa juzi.
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na viunga vyake, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema haoni mantiki na hakuna sababu ya kufanya haraka kupitisha muswada huo.
“Suala
hili linahitaji mjadala wa kina utaohusisha wadau mbali mbali,
wataalamu na wananchi kwa ujumla wake,” alisema Profesa Lipumba na
kuongeza:
“CUF
inaunga mkono jitihada za wabunge wa kambi ya upinzani kwa hatua zao
kupinga muswada huo, ambao haukujali na wala haukuzingatia maslahi ya
Taifa.”
Alisema CUF inatoa angalizo kwa Rais
Jakaya Kikwete kwamba kwa hali inavyoenda huenda akaenda kufunga Bunge
litalokuwa na Wabunge wa CCM pekee.
“Hiyo
inatokana na ukweli kwamba Spika wa Bunge amepoteza muelekeo na
ameshindwa kabisa kuliongoza Bunge kwa mujibu wa kanuni walizojiwekea
katika kutimiza wajibu,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Kwa hiyo basi, Rais Kikwete atakuwa amefuata nyayo za Rais wa Zanzibar.”
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Juni 26, mwaka huu alilivunja Baraza la Wawakilishi bila Wawakilishi wa
CUF kuwapo barazani.
Wajumbe hao walisusia Baraza hilo
kutokana na kutoridhishwa na uandikishaji wa wapigakura katima daftari
la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana
kama Biometric Voters Registrarion (BVR), wakisema kuwa uandikishaji huo
ulitawaliwa na ubabe.
Profesa Lipumba alionya kuwa kama Bunge litaendelea na mpango wake huo, basi CUF itaitisha maandamano ili kupinga muswada huo.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba
alisema kuwa Mkoa wa Kigoma unaweza kuendelea kiuchumi ikiwa utatumia
vizuri rasilimali zilizoko akitolea mfano Hifadhi ya Taifa ya Gombe
kwamba ikitumika vizuri inaweza kuingiza mapato mengi.
Alisema kwamba jiografia ya Mkoa wa
Kigoma inauruhusu kupata fursa nyingi za kuendelea kiuchumi kwa kuwa
wananchi wake wanaweza kufanya biashara na nchi zinazouzunguka za
Burundi Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
No comments:
Post a Comment