WAKATI
marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
wakitarajiwa kukutana Dar es Salaam leo kujadili mzozo wa Burundi,
wapinzani wa Rais Pierre Nkurunziza, wameapa kwa kusema kuwa ni lazima
kiongozi huyo ang’atuke madarakani.
Pamoja
na hali hiyo pia wameonya kuwa silaha zinazozagaa kwa wanamgambo nchini
humo zikusanywe kwa vile ni hatari hata kwa usalama wa nchi jirani.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Vuguvugu
linaloendesha maandamano nchini humo, Chauvineau Mugwengezo, alisema
kutano wa wakuu wa nchi za EAC ni lazima uzingatie suala hilo na
yanayoendelea nchini mwao.
Mkutano
huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Paul Kagame (Rwanda), Uhuru
Kenyatta (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) pamoja na Rais
anayelalamikiwa kwa kutaka kuwania tena muhula wa tatu wa uongozi
kinyume cha katiba ya Burundi, Pierre Nkurunziza.
Mugwengezo
alisema mkutano huo ambao utakuwa chini ya Mwenyekiti wa EAC Rais
Jakaya Kikwete, lazima uhakikishe unaweka mazingira ya uchaguzi nchini
Barundi kwa kuwashirikisha wanasiasa wote wa taifa hilo washiriki kwa
ukamilifu.
Mwenyekiti
huyo wa Vuguvugu la maandamano Burundi alisema masharti mengine ni
kuachiwa raia wote waliokamatwa na kuwekwa gerezani kwa sababu ya
kufanya maandamano pamoja na kurudishwa viongozi wa siasa waliokimbia
nchini humo kwa kuhofia kuuawa kwa sababu ya kumpinga Rais Nkurunziza.
Alisema pia ni lazima Serikali ya Burundi ikubali kuwanyang’anya silaha zote wanamgambo wa Imbonerakure nchini humo.
“Watumie mbinu zote, ziwe za siasa ama kidplomasia, wahakikishe Nkurunziza anaondoka baada ya mihula yake miwili.
“Huo
wa tatu ni kuvunja Katiba ya nchi na mkataba wa Arusha ambao Julius
Nyerere na Nelson Mandela walihakikisha unafikiwa na ukaipa Burundi
amani kwa miaka 10 sasa,” alisema.
Alisema mkataba wa Arusha na Katiba ya nchi hiyo hairuhusu mihula mitatu kwa kiongozi yeyote atakayetawala Burundi.
“Hausemi kuwa uwe umechaguliwa na wananchi wala wabunge, unasema utawala uwe wa mihula miwili, lazima hili liheshimiwe.
“Hata
kwenye Katiba ya nchi yetu inaanza kwa maneno; ‘Kwa kuzingatia Mkataba
wa Arusha’, hii ina maana kila kitu kinazingatia mkataba wa Arusha,” alisema Mugwengezo.
Alisema
nchi za Ulaya, Amerika, Umoja wa Mataifa (UN) na mataifa mengine,
yamempa ushauri Rais Nkurunziza lakini bado hataki kuusikia.
Mugwengezo
alisema hivi sasa maelfu ya watu wameikimbia nchi hiyo kutokana na
kuhofia usalama wao, hasa ikizingatiwa kuwa wanamgambo wa Imbonerakure
wanaua raia.
“Hawa
wanamgambo wa Imbonerakure wanaweza kumchapa bakora hata ofisa wa jeshi
na hakuna anayewazuia. Silaha zilizo mikononi mwao hawa wana mgambo
zinatishia hata usalama wa nchi za jirani ikiwamo Tanzania, lazima
silaha hii zitoke mikononi mwao,” alisema.
Kiongozi
huyo alimtuhumu Rais Nkurunziza kuwa anawasaidia wanamgambo wa
Imbonerakure hali ambayo inachangia kuvuruga amani ya nchi hiyo.
Alisema
baada ya kufuatilia mazungumzo ya marais hao yatakayofanyika Dar es
Salaam, watarudi Burundi kuungana na wananchi wanaoendeleza maandamano.
Burundi
imeingia kwenye machafuko baada ya CNDD-FDD kumteua Nkurunziza awania
urais kwa muhula wa tatu na hadi sasa watu zaidi ya 10 wamefariki
dunia kutokana na mapambano yanayoendelea kati ya waandamanaji na
polisi.
No comments:
Post a Comment