Muuguzi
mmoja wa zahanati ya Muungano, Chamwino, mkoani Dodoma, amekumbwa na
kashfa nzito baada ya kudaiwa kumchapa viboko mama mjamzito, wakati
akiwa katika hali ya uchungu wa kujifungua na kusababisha mtoto
aliyetaka kujifungua kufariki akiwa tumboni.
Aidha,
mama huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu
(ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, hali yake inaelezwa
kuwa mbaya.
Mwanamke
huyo, Mariamu Maroda, anadaiwa kulazwa kwenye chumba hicho kwa zaidi ya
wiki moja, ambapo pamoja na kufanyiwa upasuaji, hakufanikiwa kupata
mtoto wake akiwa hai.
Akisimulia
mkasa huo, mama mdogo wa Maroda, Joyce Charles, alisema Aprili 3, mwaka
huu Saa 12:00 jioni, walimpeleka zahanati ya Muungano akiwa na dalili
za kujifungua na kupokelewa na muuguzi aliyemfahamu kwa jina la Lucy.
“Nilishuhudia
Lucy akimchapa Maroda viboko kwenye mapaja na mgongoni, akisema ana
uwezo wa kujifungua lakini anadeka tu, nilishindwa kuingilia nikihofia
asimdhuru zaidi mwanangu, ila nilihuzunika sana,” alisema.
Alisema
muuguzi huyo alitumia fimbo tatu kumchapa mgonjwa wake, ambazo alikuwa
akizitumia kila moja inapovunjika. Alisema fimbo hizo zilipomalizika,
alianza kumfinya kwenye mapaja kwa kutumia rula.
“Kesho
yake saa 12:00 alfajiri, huku hali ya mgonjwa ikiwa mbaya, walitupatia
gari likatupeleka hospitali ya Mvumi Misheni, ambako walisema hali
aliyokuwa nayo mgonjwa wasingeiweza na kutuelekeza tumpeleke hospitali
ya rufaa, lakini walimpa mgonjwa chupa mbili za damu,” alisema.
Alisema
Maroda alifikishiwa chumba cha upasuaji na kisha alilazwa wodi namba
17, lakini miguu na tumbo vilianza kuvimba na alipochunguzwa ikabainika
ana usaha tumboni, hivyo aliamriwa arudishwe kwenye chumba cha upasuaji.
“Yaani
ukimuona, mwilini ana alama za fimbo na kufinywa. Sasa walipomfanyia
upasuaji kwa awamu ya pili, alipelekwa ICU mpaka hivi tunavyozungumza ni
zaidi ya wiki moja,” alieleza Charles.
Viongozi
wa Hospitali ya Rufaa, wenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo
walionekana ‘kurushiana mpira’ walipotakiwa kuelezea suala hilo. Hata
hivyo, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo, alikiri kuwepo
kwa mgonjwa huyo.
Awali Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Zainab Chaula, alisema hakuwa na taarifa za kina kuhusu Maroda.
Mkindo alisema walikuwa wameagiza Ofisi ya Mganga wa Wilaya wa Chamwino, kuwapelekea taarifa kuhusu suala hilo.
Alisema
pia wametaka Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa, ifahamishwe hatua
zilizochukuliwa dhidi ya mtumishi aliyedaiwa kumchapa viboko mjamzito
huyo.
“Mimi
sio msemaji, anayetakiwa kuwapa taarifa kamili ni RMO (Chaula) kwanini
awalete kwangu, nilichowaeleza ni ambacho nafahamu lakini siyo msemaji,
nashauri muende ofisini kwa matroni wa hospitali mtapata taarifa
kamili,” alisema.
Afisa
Muuguzi wa ICU, Christina Mlumba, alisema, Maroda alipelekwa ICU baada
ya kufanyiwa upasuaji na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Mdogo
wa Maroda, Silika Mkwawi alivieleza vyombo vya habari kuwa ingawa
hakuingia kwenye chumba cha kujifungulia katika zahanati ya muungano,
dada yake alipotolewa nje, muuguzi alimueleza kuwa alimchapa fimbo mbili
tu, kwa sababu ya kudeka kwake.
No comments:
Post a Comment