MWILI wa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Matui iliyoko Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, aliyedaiwa kufariki baada ya kuchapwa viboko na walimu wake, Emmanuel Mbigima (15), umefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Wakati
mwili huo unafikishwa hospitalini hapo jana asubuhi, ulikuwa umewekwa
kwenye gari la Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ukisindikizwa na baadhi
ya ndugu wa karibu wa familia ya marehemu.
Akizungumza
na waandishi wa habari hospitalini hapo, babu wa marehemu, Emmanuel
Ngowi, alisema mwili huo umeletwa hospitalini hapo kwa ajili ya
kufanyiwa vipimo ambavyo vimekosekana katika hospitali ya Wilaya ya
Kiteto.
"Mjukuu wangu alipigwa na walimu watatu tarehe 20 mwezi huu kutokana na kufeli mtihani wa somo la Kiswahili.
“Tumechukua
uamuzi wa kumleta hapa kwa sababu madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya
Kiteto, walishindwa kubaini kichwa kimeathirika kwa kiasi gani kwa kuwa
hawana vifaa vya uchunguzi vya kichwa.
“Hata
hivyo, majibu ya uchunguzi wa awali yaliyotolewa katika hospitali hiyo,
yalionyesha jicho la kulia lilivuja damu kwa ndani na pia mwili wa
marehemu ulikuwa na michubuko miguuni,” alisema Ngowi.
Naye
mjomba wa marehemu, Michael Ezekiel alisema matukio ya wanafunzi
kupigwa na kupoteza maisha yamekuwa yakijirudia shuleni hapo kwa kuwa
hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
“Mwaka
jana kuna mtoto alipigwa na mwalimu akafariki, lakini mtuhumiwa
alipelekwa mahakamani na baadaye kuachiwa kwa madai kuwa mtoto alikuwa
ni mgonjwa,” alisema.
Kwa
upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk.
Zainabu Chaula, alithibitisha kupokelewa kwa mwili huo na kusema
uchunguzi bado unaendelea.
Awali,
akizungumza na MPEKUZI baada ya mwanafunzi huyo kufariki, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Manyara, Christopher Fuime, aliwataja walimu waliohusika
katika tukio hilo na ambao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, kuwa ni
Machael Bajutta (28), Chalamilla Gereza (33) na Mwalimu Joyce Msiba
(36).
No comments:
Post a Comment