VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Tuesday, April 7, 2015

TANESCO Yaja LUKU Mpya Kukabili Tatizo la Sasa


Shirika la Umeme nchini (TANESCO) linatarajia kubadilisha mfumo wa huduma ya Lipia Umeme Kadri Utumiavyo (Luku) na kuuweka wa kisasa ili kuwaondolea usumbufu wateja wake.
 
Imeelezwa kuwa mfumo unaotumika sasa ni tatizo kutokana na mabadiliko hayo, mfumo mpya huenda ukaanza kutumika mwezi ujao. Hayo yalisemwa jana na Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin.
 
Alisema mfumo utakaowekwa, utakuwa wa kisasa na kwamba utawasaidia watumiaji kupata haraka huduma ya Luku. Alisema mfumo huo ni wa kompyuta, wa kisasa na wa haraka, utakaotibu kero wanayoipata watumiaji wa huduma ya Luku.
 
‘’Mfumo huo utakuwa una uwezo wa kuhudumia wateja wengi zaidi na kwa haraka ndani ya sekunde tatu, ikilinganishwa na mfumo wa zamani ambao ulikuwa unatumia zaidi ya dakika moja au sekunde 30,’’ alisema Severin.
 
Aliongeza maandalizi ya mfumo huo, yamekamilika na kwamba watakaokuwa wanatumia simu za mikononi na mawakala wanaouza Luku, wataendelea kutoa huduma hiyo.
 
‘’Mawakala wa MaxMalipo na simu zote za mikononi kama Tigo, Airtel, Zantel na Vodacom wataendelea kutoa huduma hiyo, lakini itakuwa kwa haraka na kwamba hakutakuwa na shida ya mitandao,’’ alisema.
 
Akizungumzia suala la kutopatikana kwa huduma ya Luku tangu juzi jioni, Severin alisema huduma hiyo haikupatikana, kutokana na tatizo la mtandao.
 
‘’Wakati mwingine simu za mikononi zinakuwa hazina tatizo la mitandao, lakini unakuta Tanesco mitandao yao ipo chini, vivyo hivyo na kwamba Tanesco inakuwa ipo sawa kwa mtandao, lakini simu zinasumbua,’’ alisema Severin.
 
Alisisitiza kuwa ili kupatikana haraka kwa huduma ya Luku, inatakiwa Tanesco na simu zote zinazotoa huduma hiyo kuwa na mitandao iliyo sawa. Hata hivyo, alisema huduma hiyo inapatikana kwa sasa.
 
Kwa muda mrefu, watumiaji wa huduma ya Luku, wamekuwa wakilalamikia uduni wa huduma, kiasi cha kuwafanya wateja wake kushindwa kuwa na umeme kwa siku kadhaa, kutokana na tatizo la kimfumo katika mitambo ya huduma za Luku.

No comments: