VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Monday, November 23, 2015

UVCCM Wakerwa na Tabia ya Wabunge wa UKAWA Kuwazomea Viongozi wa Kitaifa

UMOJA wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), umesikitishwa na vitendo vya  wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) bungeni muda mfupi kabla ya Rais Dk. Magufuli kulifungua rasmi Bunge la 11 mwishoni mwa wiki.
Wabunge hao wa Ukawa waliwazomea baadhi ya viongozi walioongozana na Rais Dk. John Magufuli na kuamriwa  na Spika wa Bunge Job Ndugai watoke nje.
Wabunge hao wa upinznai walifanya hivyo kama hatua ya   kutokubaliana na   kufutwa   Uchaguzi wa Zanzibar na kutaka atangazwe Maalim Seif Sharif Hamad kama mshindi wa uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana   na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na kufedhehesha.
“Kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge si tabia na desturi njema… Bunge si jukwaa la vituko au maigizo bali ni eneo lenye kujenga na kuonyesha ukamilifu na ustawi wa demokrasia  na umakini wa kila mbunge na vyama vyao,” alisema Shaka.
Alisema UVCCM inaona kitendo hicho kama kielelezo cha ukomo na upeo wa hekima za wabunge ambao wameaminiwa na wananchi kuwawakilisha kwenye moja ya mihimili ya dola.
“Tukio lile ni ishara na dalili tosha  ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kuwa hawana dhamira njema ya kuijenga nchi, kupigania maendeleo ya Taifa wala kuheshimu dhamana na amana  waliyokabidhiwa na wananchi kwa njia ya demokrasia ya uchaguzi,” alisema Shaka.
Alisema ni aibu iliyovuka mipaka kwa wabunge na vyama vyao kufanya kitendo hicho huku.
Alidai kitendo hicho kinaonyesha wabunge hao kupungukiwa  ukomavu wa siasa, uwerevu, maarifa na busara za kutosha.
“UVCCM tunawaomba Watanzania kukitazama kitendo hicho na kukiona kama mwanzo wa harakati za kuzorotesha maendeleo na kasi ya mafanikio iliyopangwa na serikali ya awamu ya tano,” alisema Shaka.
Alisema wanaamini viongozi na vyombo husika vitajipanga kukabiliana nao  kuzuia aibu kama hiyo isiendelee kutokea.
UVCCM pia umempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hotuba aliyoitoa katika uzinduzi rasmi wa Bunge la  11, Dodoma.
“Hotuba ya Rais Dk. Magufuli licha ya kuwa  na umakini, matarajio, matumaini, mwelekeo, dira na  vipaumbele muhimu pia imebeba  malengo mahususi katika kuwatumikia wananchi ikiwamo kuimarisha huduma za jamii,  maendeleo ya sekta ya utawala bora, haki na demokrasia, kudumisha  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na  uhusiano wa kimataifa,” alisema Shaka.

Monday, November 2, 2015

MREMA Afunguka: Sijakata Tamaa, Nitaendelea Kuwania Nafasi Mbalimbali za Kisiasa


Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amesema hata kama vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimefanikiwa kumwangusha kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, bado ana nguvu ya kuendelea kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na wala hajakata tamaa ya kukisuka upya chama chake.

Mrema aliangushwa katika kiti hicho na hasimu wake kisiasa, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, aliyevunja rekodi ya kupata kura nyingi kwa upande wa wabunge wa upinzani, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa  kura 60,187 dhidi ya 6,416 alizoambulia Mrema (TLP) aliyekuwa akishikilia jimbo hilo huku mgombea wa CCM, Innocent Shirima, akipata kura 16,097.

Alikuwa akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Kilimanjaro kuhusu majaliwa yake kisiasa, baada ya yeye na chama chake kukosa uwakilishi kwenye Bunge na Halmashauri za Wilaya. Mbali ya kupoteza kiti cha ubunge, TLP haikuambulia   hata kiti kimoja cha udiwani.

“Chama changu hakifi na wala sijakata tamaa, tutaanza moja na ninawaomba wanachama wa TLP watulie…Nitashirikiana na Rais ajaye aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), na tutakijenga chama chetu…Hata Dk. John Magufuli, anajua mimi ni mchapakazi na alinipigia debe na wananchi wakapuuza,” alisema Mrema.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, viti saba vya ubunge vimenyakuliwa na baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema na NCCR-Mageuzi, huku majimbo mawili ya Mwanga na Same Magharibi, yakiangukia CCM.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na NCCR-Mageuzi yenye mbunge mmoja mkoani  Kilimanjaro, sasa zitaunda halmashauri tano za wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo, Moshi Vijijini na Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili za Mwanga na Same.

Majimbo hayo na idadi ya kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi zitaunda halmashauri zake ni kama ifuatavyo;
Moshi Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati ya 21 na CCM imepata Kata mbili za Bondeni na Kilimanjaro, wakati Jimbo la Hai, Chadema imeshinda kata 16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya Bomang’ombe ndio pekee haijafanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM kufariki dunia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Aidha, Chadema iliyoshinda kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya Rombo, ndiyo itakayounda halmashauri ya wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi iliyoshinda kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya udiwani katika Jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja ya Wilaya ya Moshi.

Katika Jimbo la Moshi Vijijini, CCM imeshinda kata moja tu.
Mpekuzi blog