VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Friday, January 29, 2016

Waziri Mkuu: Tutahakikisha Nidhamu Inarudi Serikalini



Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa,amesema serikali imeweka msisitizo katika kuhakikisha inarudisha nidhamu kwa watumishi wa umma kwa kuweka mkazo katika uadilifu, uwajibikaji, kutoa huduma kwa wakati.

Waziri mkuu Majaliwa ameyasema hayo  katika mkutano wa pili kikao cha tatu Bungeni Mjini Dodoma alipokua akihitimisha hoja ya kujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa siku ya ufunguzi wa Bunge la kumi na moja tarehe 20 Novemba 2015 
Amesema  kuwa serikali itakuwa inawakumbusha watanzania na watendaji wa serikali  kufanya majukumu yao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka dhidi ya watumishi wanaokwenda kinyume na misingi ya utendaji kazi serikali kwa kuzingatia kauli mbiu ya hapa kazi tuu.

Pia amesema kuwa baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge ambazo utekelezaji wake utahitaji kutengewa fedha za uandalizi wa kutenga fedha za serikali na utendaji wake utafanyika kwa haraka kwa kuzingatia maombi na hoja za wabunge kwakusimamia mapato ya Taifa ili yaongezeke kwa kiwango kikubwa.

VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Thursday, January 28, 2016

Wabunge wa Upinzani Watoka Bungeni tena.......Ni Baada ya Naibu Spika Tulia Ackson Kuwanyima Muongozo ili Waongee


Hali ya sintofahamu imeendelea ndani ya bunge baada ya wabunge wote wa Upinzani kutoka ndani ya bunge mara baada ya Wabunge kuanza kuchangia hotuba ya Rais.

Baada ya  kipindi cha Maswali na Majibu, yalifuata matangazo  na   baada ya Matangazo, wabunge wakaanza kuchangia hotuba ya Rais Magufuli .

Wakati hayo yakiendelea, wabunge kadhaa wa UKAWA akiwemo mbunge wa Ubungo(chadema), Saed Kubenea walikuwa wakiomba muongo wa Naibu Spika ili waongee lakini hawakupewa nafasi.

Naibu Spika alikataa miongozo hiyo na kulitaka Bunge lijikite katika kujadili Hotuba ya Rais. Hali hiyo iliwakera wabunge wa upinzani  kwa madai kuwa wamezibwa midomo na hivyo wakaamua kutoka nje ya ukumbi wa bunge
==>Wabunge wa CCM wanaendelea  kujadili Hotuba ya Rais.
VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Tuesday, January 26, 2016

Membe Azungumzia Mpango wa Kustaafu Siasa..... Aanza Kuandika Vitabu Kama Samwel Sitta



Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hana mpango wa kustaafu siasa kwa sababu haina mwisho.

Pia, amesema kwa sasa anafanya kazi ya uandishi wa vitabu kwa lengo la kuwashirikisha na kuwarithisha Watanzania mazuri aliyonayo baada ya utumishi wake wa kisiasa wa miaka 35.

Amesema anaandaa vitabu vinne vyenye maudhui tofauti. “Hilo la kuandika vitabu nimeshalianza, nina vitabu zaidi ya 265 nimehifadhi na kuvisoma katika maktaba yangu kuhusu mambo mbalimbali ya dunia, nami ninatengeneza vinne, muda ukifika nitatoa taarifa,” alisema Membe.

Waziri huyo aliyehudumu katika Serikali ya Awamu ya Nne katika wizara hiyo kwa miaka tisa, alisema kati ya vitabu anavyoandika viwili vitatoka mwaka huu.

“Kimoja cha maisha yangu, ni vitabu vizuri sana, nimekuwa mwanasiasa kwa miaka 35, nimejihusisha zaidi na masuala ya utatuzi wa migogoro barani Afrika... kitabu kingine kitahusu migogoro na Serikali za Afrika,” alisema.

Alitaja vingine kuwa ni kuhusu uongozi na cha mwisho kitahusu siasa za Tanzania kinachowalenga zaidi vijana kikieleza namna nchi inavyoweza kulinda heshima yake duniani.

“Nchi hii tumeirithi kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Yeye alikuwa mwana ukombozi halisi. Mwaka 1963 alianzisha harakati za ukombozi, Tanzania ikawa makao makuu ya nchi zote zinazopigania uhuru. Vyama vya ukombozi vikaweka makao makuu yake hapa, vingine vikaanzia harakati zake hapa,” alisema Membe.

Alisema sifa ya kwanza ya Tanzania duniani ni ukombozi na ilikuwa mwenyekiti wa nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi Kusini mwa Afrika.

Akizungumzia kuhusu hatima yake kisiasa, Membe aliyewania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM kabla jina la Dk John Magufuli ambaye sasa ndiye rais kuteuliwa, alisisitiza kuwa siasa haina mwisho.

“Tafsiri ya siasa ni mchakato wa namna ya kuyashughulikia matatizo ya watu, usipoyashughulikia vizuri, utaibadilisha siasa kutoka kwenye amani kwenda kwenye mtafaruku,” alisema.

Akimnukuu aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, Membe alisema mwanasiasa mzuri duniani ni yule aliyeondoka kwa heshima na anayeheshimu familia yake.

Membe aliwataka wanasiasa walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuacha kujipenyeza na kuendeleza ubabe wa kisiasa, akisema kufanya hivyo ni sawa na upuuzi, badala yake wasubiri muda wao watakapochaguliwa.    
VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Tuesday, January 19, 2016

Wabunge Wote wa CCM Wakutana Dodoma Kupanga Mikakati..Nimekuwekea Picha Kadhaa Hapa


Wabunge wa CCM wakimsikiliza Mbunge wa Kibakwi Mhe. Boniface Simbachawene wakati akifafanua mambo mbali mbali kwenye ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Isimani Mhe. William Lukuvi akichangia hoja kwenye semina ya wabunge wa CCM.
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana (katikati) ambaye ndie mwenyekiti wa kikao maalum chenye kutoa semina elekezi kwa wabunge wa CCM, kulia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mhe. Philip Mangula na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye (kushoto).
Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi Mhe. Mwigulu Nchemba akifuatilia kwa makini hoja mbali mbali zilizotolewa na wabunge wa CCM kwenye semina maalum elekezi kwa ajili ya wabunge wa CCM mjini Dodoma.

VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Monday, January 18, 2016

Matokeo Ya Kidato Cha Pili Yaingia Dosari......Wamiliki Wa Shule na Vyuo Wataka Mfumo wa GPA Ufutwe



WAMILIKI wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali wameiomba Serikali kufuta mfumo wa GPA unaotumiwa na Baraza la Mitihani (Necta) kupanga madaraja ya mitihani ya sekondari, kwa maelezo kuwa haufai kwa kuwa unahalalisha watahiniwa waliofeli waonekane wamefaulu.
Akizungumza jana Dar es Salaam kuhusu matokeo ya kidato cha pili ambayo yametangazwa na Necta hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alisema matokeo hayo hayaeleweki kwani wameshuhudia baadhi ya wanafunzi wanaoonekana kufanya vizuri chini ya mfumo wa GPA wakati katika mfumo wa madaraja (division) wanaonekana wamefanya vibaya.
Kwa hali hiyo, Nkonya amemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kufuta mfumo huo hadi pale Necta itakapokuwa tayari kujibu maswali kadhaa ya wadau wa elimu ambao wanaona mfumo huo hauna tija katika kuboresha elimu.
Baadhi ya hoja ambazo zilihojiwa na Nkonya ni kwamba kulikuwa na kasoro gani katika mfumo wa madaraja mpaka ukaja huo wa GPA na akataka kujua ni nani alilalamikia mfumo wa division mpaka ukaondolewa? Alihoji kabla ya mfumo huo kuletwa, ni wadau wapi walishirikishwa?
Alisema TAMONGSCO ilipata taarifa za kuwepo kwa mfumo huo wa GPA kupitia vyombo vya habari na hawakushiriki katika ngazi yoyote ya mijadala ya kisera kama sheria inavyoelekeza. 
Katibu Mkuu huyo wa TAMONGSCO alihoji, “Je, alama za chini za gredi D, C,B na A zilibaki kama zilivyokuwa wakati wa mfumo wa division au kuongeza gredi E na B+ ilikuwa mbinu ya kushusha alama za ufaulu na matumizi ya GPA yakaanzishwa kwa lengo la kuficha ukweli kuwa viwango vimeshushwa kwa kiasi kikubwa??
Nkonya pia alihoji mfumo huo una faida zipi na unasaidiaje katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza wanakuwa na ujuzi stahiki utakaowawezesha kuhimili changamoto za soko la ajira na utandawazi?
“Kwa hali hii bado tunaishauri Serikali isitishe matumizi ya mfumo wa GPA hadi pale hoja zetu zitakapopatiwa ufumbuzi,”alisema Nkonya.


VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Sunday, January 17, 2016

TCRA Yavifungia Vituo 27 Vya Radio Na Tv Kwa Kukwepa Kodi.......Miongoni Mwa Vituo Vilivyofungiwa ni Star Tv, Radio Free Africa na Kiss Fm



Mamlaka ya Mawasiliano TCRA imevifungia vituo 21 vya Radio na 6 vya TV kikiwemo kituo cha Star TVRadio free AfrikaKiss Fm na Uhuru FM kwa kushindwa kulipa kodi ya lesseni kwa wakati ..
Akitangaza uamuzi huo, mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy, amesema kuwa mitambo ya vituo hivyo itazimwa ifikapo kesho saa 6 usiku, na itawashwa baada ya vituo hivyo kulipa madeni yanayowakabili.
Mungy amesema mamlaka hiyo haiwezi kusema ni kiasi gani cha pesa ambacho vituo hivyo vinadaiwa kwa madai kuwa kanuni na taratibu haziwaruhusu kutaja kiasi hicho kwa kuwa ni siri kati ya TCRA na mteja.
Aidha Mungy amesema kuwa TCRA imewataka wadau wote wa mawasiliano nchini kutii sheria bila shuruti na kufuata taratibu, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo la kuwasaka wanaokwepa kodi ni endelevu.
==> Vituo vingine vilivyofungiwa ni;
Sibuka FM Breez FM Country FM Ebony FM Hot FM Impact FM Iringa Municipal TV Kiss FM Kitulo FM Kifimbo FM Mbeya City Municipal TV Radio 5Radio Free Afrika (RFA)Musa Television NetworkPride FM radioRadio HurumaRadio UhuruStar TVRock FM RadioStandard FM radioSumbawanga Municipal TVTanga City TVTop Radio FM limitedUlanga FM 

VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Thursday, January 14, 2016

ZOEZI LA KUWASAKA WAHAMIAJI HARAMU LAPAMBA MOTO MKOANI MBEYA




Afisa Uhamiaji  Mkoa wa Mbeya Ndugu Asumsyo Achacha akizungumza ofisni kwekwe juu ya zoezi linaloendelea la kuwasaka wahamiaji haramu mkoani humo.
Na jamiimojablogu,Mbeya
Zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu na wageni wanaofanya kazi bila kibali limeendelea kufanikiwa mkoani Mbeya ambapo jumla ya wageni 20 wamekamatwa mkoani humo kutokana na makosa mbalimbali likiwemo la kuingia nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwakwe Afisa uhamiaji Mkoa wa mbeya Ndugu Asumsyo Achacha amesema hatua hiyo imefanyika ikiwa ni kutekeleza majukumu yao ya kila siku sanjali na kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt Charles Kitwanga alilotoa hivi karibuni.
Aidha amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria mpya  ya kuratibu ajira za wageni ,Sherii Na.1 ya mwaka 2015 ambayo inawataka wageni wote walioajiliwa hapa nchini kuwa na vibali vya kazi na hati za ukaazi nchini.
Afisa uhamiaji huyo amewataja raia hao waliokamatwa katika msako huo ni pamoja wakenya watatu (3)wamalawi 14 pamoja na wakongo watatu (3).
Aidha amesema kuwa mwaka 2015 jumla ya wahamiaji haramu 478 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali  ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na kufukuzwa nchini.
Amesema mbali na changamoto zilizojitokeza ikiwemo upungufu wa vitendea kazi ,fedha pamoja na rasilimali  bado shughuli za uhamiaji mkoani humo ziliendelea kufanyika kama kawaida na kwa ufanisi mkubwa.
Pia Afisa Uhamiaji huyo amebainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo ofisi yake itahakikisha kila mtu aliyevunja sheria anakamatwa hivyo ametoa wito kwa waajiri kuacha tabia ya kuwapa ajira wafanyakazi wa kigeni wasio na vibali vya kazi na ukaazi kwani msako huo utaendelea katika viwanda ,migodi mashuleni na mahotelini.


VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Monday, January 11, 2016

Rais Magufuli Amjulia Hali Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye Aliyelazwa Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili Januari 11,2015


Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimpa pole Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Freredick Sumaye alipokwenda kumjulia hali katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam Januari 11, 2016 
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Freredick Sumaye na Mama Esther Sumaye alipokwenda kumjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu huyo Mhe Freredick Sumaye katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam Januari 11, 2016

VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Sunday, January 10, 2016

David Kafulila ...Afunguliwa Kesi Nyingine Kigoma..Mwenyewe Adai ni Hujuma...


Taarifa ninayokusogezea ni ya David Kafulila aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, tunafahamu ana kesi Mahakamani ya kupinga matokeo ya ubunge 2015 jimbo la Kigoma Kusini kesi ipo Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, taarifa ikufikie kuwa Kafulila baada ya kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma akasomewa kesi mpya ambayo anakiri hakuwa anaifahamu mwanzo kwenye sentensi zake;

Nilifikishwa mahakamani kwa kesi mpya ukiachilia kesi ya kwanza ya kupinga matokeo ya uchaguzi 2015 jimbo la Kigoma kusini, awali nilikuwa nikijua ninakesi moja katika mahakama ya hakimu mkazi kigoma kwa madai kwamba nilimdhalilisha aliyekuwa mkuu wa wilaya Khadija Nyembo tangu mwaka 2013….nikiwa mahakamani nikapewa tena kesi nyingine ni kesi ya kuhamasisha wananchi wasichangie mchango wa maabara; – David Kafulila

Bado msimamo wagu utabaki palepale kwamba nitaendelea kupigania nchi yangu, kesi hizi zote katika mahakama ya hakimu mkazi Kigoma ukitazama hati za mashitaka yote ya Kafulila hapa Kigoma zimeandaliwa na kusainia na DPP makao makuu Dar es salam inawezekanaje;- Kafulila        VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Friday, January 8, 2016

Rais Benjamin Mkapa Naye Ataka Kutumbua Majipu, Amwambia Rais Magufuli Haya Hapa..

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amesema yuko tayari kutoa ushirikiano wa kila aina au kufanya kazi yoyote endapo Rais Dk. John Magufuli atahitaji.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Mkapa alitoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo Ikulu na Rais Magufuli.

Ilisema lengo la Mkapa kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi, kuunda Serikali na kumtakia heri ya mwaka mpya.

Mkapa amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo,” ilisema taarifa hiyo.

Pia Rais Magufuli alikutana na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba ambaye alisema Watanzania wote wanapaswa kumuunga mkono kiongozi huyo kwa kazi kubwa anazofanya ambazo ni kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali za umma.

Lazima kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuachia, pale ulipo kama ni mambo ya rushwa uanzie hapo hapo, mambo ya matumizi mabaya ya madaraka anzia hapohapo, tusije tukamuachia Rais peke yake… yeye awe kiongozi wetu, lakini Watanzania wote tushughulike na matatizo hayo,” ilisema taarifa hiyo ikimkariri Jaji Warioba.

Pamoja na kumtakia heri ya mwaka mpya, Jaji Warioba alimpongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri, hususani katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi ikiwamo afya na maji.
Kauli ya Mkapa na Jaji Warioba imekuja siku moja tu baada ya juzi Rais mstaafu Jakaya Kikwete kumtembelea Rais Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo ambayo hata hivyo yameendelea kuwa ni siri.

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wastaafu ndani ya siku mbili kumtembelea Rais Magufuli tangu ameingia Ikulu Novemba 5, mwaka jana.


VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......

Mwanamke Afia 'Gesti' Akiwa na Mchepuko


Mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa)  anayedaiwa ni mke wa mtu, amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya Bukoba, akiwa na mwanaume mwingine anayesemekana ni hawara yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, watu hao walienda katika nyumba hiyo ya kulala wageni iliyopo eneo la Hamugembe Januari 3, mwaka huu na kuchukua chumba namba nane.

Alisema siku iliyofuata saa 6:00 mchana, polisi walipokea taarifa kutoka kwa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuwa katika chumba hicho kuna watu waliingia jana yake lakini hadi muda huo mlango wa chumba ulikuwa haujafunguliwa na kuna ukimya uliowatia hofu.

Alisema wahudumu hao waliambatana na polisi na walipofika eneo la nyumba hiyo walimkuta mmiliki wake ambaye alitoa funguo za akiba na kufungua chumba hicho.

“Polisi walipofungua chumba walikuta godoro liko chini lakini kitandani lilipopaswa kuwa kulikuwa na mwili wa mwanamke ukiwa umefunikwa shuka na kuuchukua kwenda kuuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera,” alisema.

Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Kagera, alisema mtu aliyekuwa pamoja na mwanamke huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni dereva wa basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Bukoba na Mwanza, hakukutwa katika chumba hicho na alifunga mlango kwa nje na kuondoka na funguo.
Hata hiyo, alisema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana lakini kutokana na taarifa walizopata kutoka kwa msaidizi wa dereva huyo wamefanikiwa kumpata mtu aliyejitambulisha kuwa ni mume wa marehemu.

Kamanda Ollomi aliongeza kusema kuwa,  mume wa marehemu mkazi wa Butimba, jijini Mwanza, amepatikana na kukabidhiwa mwili wa mkewe, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea na kwamba wafanyakazi wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi lakini pia kwa kitendo cha kuficha taarifa za wageni wanaolala katika nyumba hiyo.



VITUS MTAFYA ..... ILEJE NI NYUMBANI ......