VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Wednesday, September 16, 2015

Kati ya Magufuli na Lowassa, ni Nani atatufaa Kwa siasa za Nje?


“Msifanye mabadiliko kwa pupa kama watu wa Libya. Walimuondoa madarakani rais Saddam, hapana rais Gaddafi maana Saddam alikuwa rais wa Kuwait!!”.

Sikuamini masikio yangu kwamba haya ni maneno yaliyotoka kinywani mwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Pombe Magufuli.

Alikuwa akiongea na wananchi wa Tanga katika mkutano wa kampeni akiwahadharisha Watanzania wasivichague vyama vya upinzani, kwa lengo la kufanya mabadiliko kwa sababu kufanya hivyo ni kuchagua bora mabadiliko wakati mabadiliko bora yatapatikana.

Nia yangu siyo kumfedhehesha mgombea huyu anayesifika kwa uadilifu na uchapakazi, lakini hivi kuna asiyejua kuwa Saddam Hussein hakuwa rais wa Kuwait bali Iraq? Kila mtu anajua hivyo, nashangaa tu kwamba mgombea wangu wa urais ama kweli hajui hili au hayuko makini katika masuala ya kimataifa.

Ninachokusudia ni kujaribu kuwahadharisha Watanzania kwamba zama hizi rais wa nchi haongozi ndani ya mipaka ya nchi hiyo pekee, bali anakuwa kiungo muhimu kati ya nchi yake na jamii ya kimataifa katika ulimwengu huu ambao sasa ni kama kijiji.

Moja ya mafanikio ya rais wa nchi yeyote ile duniani ni jinsi gani anazicheza karata zake kwenye medani ya kimataifa. Siasa za kimataifa siku hizi ni mchezo hatari, kiasi kwamba kama rais hazijui vizuri siasa za kimataifa kuna hatari ya kushindwa kutekeleza ilani na sera za chama chake awapo madarakani, kwa sababu ya misuguano na wale waitwao washirika wa maendeleo ambao ni nchi zilizoendelea.

Ukubwa wa hatari hii unazidi pale nchi yetu inapoingia katika uchumi wa mafuta na gesi asilia. Rasilimali mbili hizi zimeyaingiza mataifa yenye rasilimali hizo katika machafuko.

Kwa mujibu wa andiko, Oil and Diamonds as causes of civil war in sub-Saharan Africa, rasilimali ya mafuta na gesi zinaweza kuitia nchi katika machafuko. Lakini hilo hutegemea wingi wa rasilimali hiyo, sera na mikataba ya nchi husika kwa mataifa na mashirika wahitaji wa rasilimali hiyo kwa lugha rahisi wawekezaji.

Jingine ni uwezo wa kidiplomasia ya uchumi wa viongozi wa nchi yenye rasilimali kumudu hila, njama, migandamizo na vishawishi vya wawekezaji hao. Kwa maneno mengine, uwezo wa rais aliye madarakani katika kuongoza diplomasia na mataifa ya nje.

Mbali na rasilimali, uwezo wa rais katika diplomasia na mataifa ya nje ni mtaji muhimu katika kuvutia wawekezaji katika kile kijulikanacho kama mitaji ya moja kwa moja kutoka nje au ‘foreign direct investment (FDI)’, misaada mbalimbali kwa nchi na hata haiba ya nchi kimataifa.

Kwa kweli Rais wa Tanzania anayemaliza muda wake ameipaisha Tanzania katika medani ya kimataifa, ingawa mwishoni mwa utawala wake mataifa na wadau wa maendeleo walifikia kuzuia misaada yao kupinga kashfa mbalimbali, ikiwamo kashfa ya Tegeta Escrow iliyolitikisa Taifa.

Hatari iliyoko mkipata rais asiyejua changamoto zinazolikabili taifa katika siasa za kimataifa ni kuchukua maamuzi yanayoweza kuliingiza taifa katika hasara na hata katika migogoro ya ndani na nje.

John Perkins anaandika katika kitabu chake “The confession of an economic hitman” kwamba mashirika ya kimataifa hususan yale ya uchimbaji mafuta na gesi, huyaingiza mataifa katika lindi la madeni, umaskini na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa kuwapima wagombea wetu ili kuona ni nani anafaa kwa siasa za nje?
 
 Mwandishi wa makala katika gazeti mmoja litokalo kila siku hapa nchini, alimsifia Dk John Magufuli kwamba katika kipindi chake cha miaka 20 ya utumishi serikalini, amesafiri kwenda nje ya nchi mara nne !

Hii inaonyesha kuwa si mtu mbadhirifu kwani uchache wa safari za nje unathibitisha kuwa yeye siyo mwenye kufanya matumizi ya ovyo ovyo. Japo hili ni jambo zuri kwa upande mmoja, kwa upande wa kukuza uelewa wake katika medani za kimataifa, si jambo la kujivunia. Ziara za nje hupanua uelewa wa mtu katika diplomasia ya kimataifa.

Magufuli Vs Lowassa

Kupitia hotuba zake za kampeni mtu anaweza kupata wasiwasi juu ya uwezo wa Dk Magufuli kuhusu siasa za nje. Ule mfano wake maarufu wa kulinganisha mabadiliko ya Tanzania na yale yaliyotokea Libya umetoa picha hasi kwamba hajui vyema siasa za kimataifa.

Ukichanganya na kauli yake “mimi sifanyagi (sifanyi) siasa na kwa bahati mbaya naweza kuwa si mwanasiasa mzuri,” unapata shaka kama kweli atamudu siasa za kimataifa zilizojaa ulaghai, hila na mizengwe dhidi ya nchi changa. Ili kuwa rais zama hizi, inabidi uzijue vizuri siyo siasa za ndani bali hata zile za kimataifa.

Hili la kutokujua au kujichanganya kuhusu Saddam alikuwa rais wa nchi gani linaweza kuonekana jambo dogo, lakini kwa watu makini haiwezekani kwa mtu msomi wa kiwango cha uzamili tena aliyekuwa katika uongozi wa nchi kama waziri kwa muda mrefu, awe hajui Saddam alikuwa rais wa nchi gani. Ni dalili kwamba kuna upungufu mkubwa kwenye uelewa wa mambo ya kimataifa kwa mgombea wetu huyu.

Lowassa kwa upande wake hatujamsikia akizungumzia lolote kuhusu masuala ya kimataifa, licha ya kuwa amewahi kuwa Waziri Mkuu na waziri wa kawaida kwa miaka mingi.

Nafasi hiyo bila shaka ilimpa uzoefu fulani katika medani ya kimataifa, kwa kuwa Waziri Mkuu ni msaidizi wa karibu wa rais kwenye mambo yote likiwamo la ushirikiano wa kimataifa. Aidha, Lowassa amesafiri mara nyingi nje ya nchi jambo linalompa fursa ya uelewa mpana kuhusu masuala ya nchi za nje.

Katika kampeni zake, tumemsikia akisema “sitosubiri misaada kutoka nje”. Hii ni kauli nzito kwa kuwa nchi hizi changa kama Tanzania haziwezi kabisa kuepuka misaada kutoka nje, ingawa pia hazitakiwi kuwa tegemezi kwani zina rasilimali nyingi.

Kuwa kwake Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), bila shaka kulimwezesha kukutana na wanadiplomasia wengi wa kimataifa wakiwamo mabalozi, mawaziri wakuu, makamu wa marais na hata marais waliowahi kuhudhuria mikutano ya kimataifa katika ukumbi huo.

Tukumbuke kwamba, mchakato wa Ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, utakuwa unaingia katika kipindi nyeti cha ushuru wa pamoja wa forodha na mamabo mengine ambapo masilahi ya nchi yetu itabidi yalindwe ipasavyo.

Ni wazi marais wa nchi jirani wanasubiri kwa hamu ni nani ataibuka Rais wa Tanzania, nchi ambayo ‘kistratejia’ imekaa vizuri kuliko nchi zote za Afrika Mashariki, lakini isiyokuwa na mikakati mizuri ya kufaidika na uwepo wake kijiografia.

Mataifa na mashirika ya nje kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na mengineyo yatakuwa yanafuatilia kwa karibu uchaguzi wa Tanzania. Kwa hiyo wakati tukishangilia kauli za wagombea kuhusu jinsi watakavyoendesha siasa za ndani ya nchi, tusisahau kuna siasa za kimataifa ambazo zinaweza kukwamisha hata mipango yetu ya maendeleo, iwapo rais atakayechaguliwa hatokuwa na uzoefu au uelewa wa kutosha. 
 

No comments: