VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Monday, February 2, 2015

MADIWANI MBEYA VIJIJINI, WAMTIMUA OFISA ELIMU. NI KUTOKANA NA MATOKEA DARASA LA SABA



 MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Vijijini, wamefikia makubaliano ya pamoja kumwondoa kwenye nafasi yake afisa elimu shule za Msingi wa wilaya hiyo, Dionis Boay, kutokana na Halmashauri hiyo kushika nafasi ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba.
Maazimio hayo yalifikiwa jana katika kikao cha Baraza la madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmshauri hiyo.
Pamoja na mijadala mingine, lilipofika suala la elimu, Afisa elimu huyo alisimama na kuwasilisha taarifa ya elimu na jinsi idara yake inavyojipanga kufuta aibu ya kushuka kwa ufaulu katika wilaya hiyo, ndipo diwani wa kata ya Masoko, Edward Mwampamba(Chadema), aliposimama na kusema kuwa chanzo cha matokeo mabaya katika wilaya hiyo ni maafisa elimu.
(Maafisa elimu ndiyo chanzo cha ufaulu mbaya katika wilaya yetu, hususani katika kata yangu, kuna walimu saba wamehamishwa na hawataki kuleta walimu wengine” alisema Mwampamba na kuwataja majina walimu hao.

Diwani wa kata ya Ilungu, Hashim Mwashang’ombe, alisema kuwa kutokana na Halmashauri hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, anahitaji afisa elimu na jopo lake la taaluma ngazi ya wilaya wapishe ofisi hizo kuanzia jana.
Akiwa anaendelea kuwashawishi madiwani wenzake kukubaliana na hoja yake, ndipo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Andason Kabenga, alipochukua kipaza sauti na kusema kuwa jambo hilo halipaswi kuchukuliwa mzaha na kupoteza muda kulijadili bali Afisa elimu huyo na timu yake wanapaswa kuondolewa haraka.
“Sioni kuwa hili ni jambo la kujadili kwa muda mrefu, bali afisa elimu anapaswa kuondolewa kwenye nafasi hiyo na wenzake” alisema Kabenga huku madiwani wakipiga makofi na kwamba hawawezi kuendelea kucheka na nyani.
  

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya, Upendo Sanga.(Picha na maktaba)
Baada ya maazimia hayo ya madiwani kuhusu afisa elimu huyo na jopo lake ngazi ya wilaya, ndipo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Upendo Sanga, aliposoma sheria na kuomba waalikwa kuwapisha madiwani na kugeuza Baraza hilo kuwa kikao.
Mbali na jambo hilo, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Mch. Luckson Mwanjale, alibanwa na baadhi ya madiwani kuwa aeleze kwanini anatoa ahadi kwa wananchi na kuzitumia fedha za mfuko wa jimbo bila kukaa kwanza na kamati ya fedha.

Akitoa majibu ya swali hilo, Mbunge huyo alisema kuwa, sheria za matumizi ya mfuko wa jimbo zipo wazi ikiwemo kuwaambia wananchi kupeleka barua ofisini kwake kabla ya kuwaahidi kutatua shida za maendeleo au kuwaahidi hata kabla ya barua na kufika katika kamati ya fedha.

No comments: