VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Thursday, March 26, 2015

Lowassa Amjibu Nape Nnauye.....Ahoji ni Kikao gani Cha Chama Kilichomtuma Kutoa Tamko??....Apokea Maandamano ya Vijana 60 Toka Mbeya Wakimtaka Agombee Urais


SIKU  moja baada Katibu wa itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye kutoa kauli ya chama hicho kuhusu makundi yanayojitokeza kumshawishi waziri mkuu mstaafu Mhe Edward Lowassa kugombea urais, kuwa yanaweza kumkosesha sifa kiongozi huyo ya kuwania nafasi hiyo, Mh. Lowassa amejibu kauli hiyo na kudai anashangazwa nayo huku akihoji imetokana na maamuzi ya kikao gani ndani ya CCM.
 
Lowassa  amedai kuwa hana njia ya kuwazuia watu wasimuombe agombee Urais  na ametoa  ombi kwa wale wote ambao bado wana nia ya kumshawishi agombee nafasi hiyo ya urais, wasubiri kwanza hadi pale chama chake hicho kitakapotoa maelekezo.
 
Akizungumza na vijana 60 wa bodaboda kutoka wilaya ya Mbarali, Mbeya waliokwenda pia kumshawishi agombee nafasi hiyo, mjini Dodoma jana, alisema si vyema kwa maofisa wa chama kuzungumzia masuala ya wanachama wao kwenye vyombo vya habari wakati kuna vikao vya chama.
 
Alisema watu waliojitokeza na kumshawishi kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ya Urais, hajawaita wala kuwalipa chochote kama inavyodaiwa na kwamba walikuwa wakifuata maneno ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa mkoani Ruvuma katika sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya Uhuru.
 
Alisema katika siku hiyo, Rais Kikwete aliwataka watanzania wawashawishi viongozi wanaoona wanafaa ili wajitokeze kugombea nafasi hiyo ya Urais.
 
“Mimi ni vigumu kuzuia mafuriko kwa mikono. Nazuia mafuriko kwa mikono, yanakuja mimi nayazuia kwa mikono, nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema Lowasa.
 
Alisema tangu makundi hayo yaanze kujitokeza kumshawishi kuchukua fomu mambo mengi ya ajabu yamesemwa jambo ambalo linamsikitisha na kumshangaza kwa kuwa endapo kuna mtu wa chama mwenye hoja, ni vyema kuwasilisha kwenye vikao vya chama badala ya kuzungumza hadharani na kwenye vyombo vya habari.
 
Alisema mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama, ambapo majadiliano hufanyika na mwisho wa siku watu huelewana na kamwe mambo yanayohusu chama yahawezi kuzungumziwa kwenye vyombo vya habari., televisheni na redio jambo ambalo ni hatari sana.
 
“Niseme mawili tu yanayonisikitisha, wanasema mnakuja nimewaiteni ninawapa fedha, hela za kuwapa ninazitoa wapi? Mkija hapa nikiwawekea maturubai ni kosa, mkiwa na viti ni makosa na wanasema nawapikieni chakula, mambo ya ajabu sana,” alisema.
 
Alisema juzi vijana takribani 300 walimtembelea nyumbani kwake, na kushangaa ni namna ipi angeweza kuwapikia chakula vijana wote hao.
 
“Ni vibaya sana kumdhalilisha mwenzako kwamba maisha yake yote akili yake ni kufikiria tumbo, huyu hana cha kufikiria isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowasa awape chakula, ni kudhalilisha watu,” Alisema watu waliomtembelea walikwenda kwa utashi wao wenyewe, kwa gharama zao.
 
“Sijawaona, sijawatuma, ama mmeniona huko? Nimekuja kuwashawishi? Nimewahi kuja huko Mbarali kuwashawishi mje kwangu? Au nimewapeni hela leo mlipokuja hapa, hata soda zenyewe hamjanywa.”
 
Aliwataka wale ambao wanapanga kumshawishi waache kwanza hadi wapate maelekezo ya chama ili kuepusha migogoro kwenye chama hicho.
 
“Nina uhakika tutapata nafasi, jambo moja ninataka kuwapa matumaini ipo siku watanzania watapata uhuru wa kusema juu ya mtu, iko siku watapiga kura zao kusema kwa hiyo tungojee hiyo siku.
 
"Nina uhakika wapo watanzania wengi wanaonipenda kama walivyosema kwa kazi zangu, watapata nafasi ya kusema naam ama hapana, kwa hiyo huyo anayepiga kelele nyingi sijui nitoke chama sijui nifanye kitu gani angoje wanaCCM na watanzania waamue,” alisisitiza.
 
Alisema kitendo cha kufuatwa na makundi mbalimbali ya watanzania kumshawishi kuwania nafasi ya Urais, kinatokana na ukweli kuwa anaaminika na kupendwa kutokana na mambo mengi aliyoyafanya.
 
Kwa takribani wiki nzima sasa, Lowasa amekua akipokea makundi mbalimbali ya watu wakiwemo wazee wa CCM, mashehe kutoka Bagamoyo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na jana waendesha bodaboda kutoka Mbarali wakimtaka achukue fomu kuwania urais.

Edward Lowassa akisalimiana na Kamanda wa Vijana Wilaya ya Mbarali ambaye ni Mfanya Biashara, Ibrahim Ismail Mwakabwangas alipowasili eneo hilo na ujumbe wake.
Ibrahim Mwakabwangas akizungumza. 
Lowassa akipokea salama hizo.
Mwenyekiti wa Bodaboda Mbarali, Yahya Katagara akizungumza.
Kamanda wa Vijana Ibrahim Ismail Mwakabwangas akizungumza na makada wake.
Lowassa akiagana na ujumbe huo.

No comments: