VITUS BENEDICTO MTAFYA

SPORT AND GAMES

Tuesday, December 9, 2014

Daktari feki akamatwa Tanzania

Sekta ya afya nchini Tanzania bado inakabiliwa na tatizo la madaktari feki ambapo jana Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu, MOI ilimkamata daktari feki aliyefahamika kwa jina la Dismas John Macha mwenye umri wa miaka 35.

Taasisi hiyo ipo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, MNH jijini Dar es Salaam, ambapo daktari huyo anadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kwa madai kwamba angemhudumia mgonjwa wao.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Mkurugenzi wa MOI, Athumani Kiloloma, alisema mara ya kwanza alikamatwa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS, akijifanya mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika shule ya tiba.
Dk. Kiloloma alisema alipokamatwa mara ya kwanza, walitoa matangazo katika hospitali nzima na kutoa taarifa kwa wananchi, lakini wanashangaa tukio hilo limejirudia tena.

Akizungumzia tukio hilo, mkurugenzi huyo alisema wanakabiliwa na tatizo kubwa la madaktari feki, ambao wamekuwa wakiomba michango mbalimbali ya fedha.

Mtuhumiwa Dismas Macha anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
Awali, Dismas akizungumza na waandishi wa habari, alisema yeye si daktari bali ni mgonjwa wa akili.

Matukio ya madaktari feki yamekuwa yakiripotiwa katika hospitali mbalimbali nchini Tanzania katika siku za karibuni, ambapo inadaiwa madaktari hao kazi kubwa ni kuwatapeli wagonjwa na ndugu wa wagonjwa.

No comments: